Ronaldinho kuoa wake wawili kwa pamoja

UNATAKA kushangaa, nenda kashangae baharini huko, shilingi ndogo inazama, meli kubwaaa inaelea! Unajua kwanini, iko hivyo? Basi utashangaa mengi likiwamo hili la supastaa wa Kibrazili, Ronaldinho amepanga kufunga ndoa na wanawake wawili kwa pamoja huko kwao Brazil.

Taarifa zinafichua Ronaldinho amepanga kuwaoa wachumba zake hao wawili, Priscilla Coelho na Beatriz Souza Agosti mwaka huu baada ya kuishi nao kama vimada kuanzia Desemba mwaka jana. Ronaldinho aliishi na wanawake hao ambao hivi punde watakuwa wake wenza huko kwenye jumba lake lenye thamani ya Pauni 5 milioni lililopo katika jiji la Rio de Janeiro. Ronaldinho alianza kudeti na Beatriz mwaka 2016, lakini wakati huo akiwa kwenye uhusiano na Priscilla, ambaye hakutaka kumtema na kuendeleza mahaba naye. Ripoti zinadai wachumba hao wawili wote wamekuwa wakipewa pesa Pauni 1,500 kwa kadiri wanavyotaka wenyewe.

Ronaldinho anaripotiwa hata zawadi anazowapa wanawake hao wawili huwa zinafanana, kwamba pafyumu anayojipulizia mmoja, basi na mwingine ni ya aina hiyo hiyo.