Rashford fimbo ya Mourinho kwa vigogo

Muktasari:

Mshambuliaji huyo sasa amewatisha mabeki wa timu pinzani baada ya kuwaambia kuwa ameanza kumwelewa vizuri Jose Mourinho kwa kile anachomtaka akafanye uwanjani wakati anapompanga kikosini.

London, England. Tangu anaibukia kwenye kikosi cha Manchester United, mshambuliaji Marcus Rashford amekuwa kiboko ya Big Six, akizipiga mabao mara nyingi tu, ukiiweka kando Liverpool kwa kile alichowafanya Jumamosi iliyopita.
Mshambuliaji huyo sasa amewatisha mabeki wa timu pinzani baada ya kuwaambia kuwa ameanza kumwelewa vizuri Jose Mourinho kwa kile anachomtaka akafanye uwanjani wakati anapompanga kikosini.
Siku za karibuni, Rashford alikuwa akisugua tu benchi na hakuwa ameanzishwa mechi yoyote kwenye Ligi Kuu England tangu mwaka huu uanze hadi hapo Jumamosi iliyopita, alipoanzishwa dhidi ya Liverpool huku Old Trafford na kufunga mabao yote mawili yaliyoipa timu yake ushindi wa mabao 2-1. Ujio wa Alexis Sanchez kwenye kikosi hicho uliripotiwa kumtibulia Rashford, lakini sasa amesema tangu akiwa benchi, amekuwa akiyafanyia kazi maelekezo yote anayoagizwa na Mourinho na sasa matunda yameanza kuonekana.
Kwenye mechi dhidi ya Liverpool, Sanchez aliingizwa kati kucheza nyuma ya Romelu Lukaku na hivyo Rashford kupata nafasi ya kucheza upande wa kushoto, ambao lilitumia vyema kufunga mabao hayo. Kwa miaka yake miwili tangu alipoibukia, kwanza alipokuwa kwenye kikosi cha Louis van Gaal na sasa, Mourinho, fowadi huyo, Rashford alisema bado yupo kwenye mafunzo ya kukiendeleza kiwango chake na hivi karibuni atakuwa amekwiva.
"Kwa sasa sijifunzi sana uwanjani kwenye mechi. Najivunza huko mazoezini," alisema.
"Kuna mambo mengi naanza kuyaelewa sasa. Kila kitu kinachohusu huu mchezo. Kocha anapenda vitu kuwa wazi. Unapokuelekeza na kwenda kuvifanyia kazi ipasavyo, basi matokeo yanakuja kirahisi sana uwanjani."
Rashford aliulizwa kama Mourinho ameshawahi kuzungumzia chochote kutokana na kutompa muda wa kutosha wa kucheza. Alijibu hivi: "Hapaswi kufanya hivyo. Kwenye soka kuna nyakati unakuwa juu na nyakati unashuka. Kitu muhimu ni kujishirikisha tu na wenzako. Kila mtu anakuwa vizuri sana mazoezini."
Kwa msimu huu, Rashford amefunga mabao 12 katika mechi 40 alizocheza kwenye michuano yote, huku akitikisa nyavu mara sita kwenye Ligi Kuu England. Kwenye Ligi Kuu England amehusika kwenye mabao 11, akifunga sita na kuasisti matano.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya amefunga mabao matatu na kuasisti mara moja, wakati kwenye Kombe la Ligi amefunga mabao mawili na asisti mbili, kwenye kwenye Kombe la FA amefunga bao moja.
Rashford ni hatari kwa kuzichapa Big Six, ambapo amefunga mabao matano katika dakika 204 alizocheza dhidi ya wababe hao kwenye Ligi Kuu England.