Povu, Guardiola ainunia tuzo ya Salah

Muktasari:

Na kweli amechaguliwa kuwa mwanasoka bora wa England msimu huu, lakini mtu mmoja amegoma.

LONDON, ENGLAND. MAWAZO ya wengi yaliamini kwamba staa wa Liverpool, Mohamed Salah angekuwa mwanasoka bora wa England msimu huu. Na kweli amechaguliwa kuwa mwanasoka bora wa England msimu huu, lakini mtu mmoja amegoma.

Pep Guardiola, kocha wa Manchester City amesisitiza kwamba staa wa timu yake, Kevin De Bruyne alipaswa kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa England msimu huu, tena kwa urahisi tu badala ya Mohamed Salah.

Staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji alifunga bao lake la 12 la msimu kwa shuti kali katika pambano dhidi ya Swansea juzi muda mchache kabla ya Salah kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu, lakini Gurdiola anaamini kwamba pamoja na Salah kufunga mabao mengi msimu huu lakini De Bruyne ni bora zaidi.

“Najua maoni yangu kuhusu tuzo hizi. Kwa mtazamo wangu, unapochambua miezi 10 iliyopita hakuna mchezaji aliye bora zaidi ya De Bruyne kwa maana ya mwendelezo wa ubora. Labda kwa namba (idadi ya mabao) kuna wachezaji wengi bora zaidi yake lakini hakuna mchezaji bora zaidi yake msimu huu. Kwangu mimi alikuwa bora sana.” alisema Guardiola.

“Ningpenda kuona anastahili, lakini katika kipindi cha majira ya joto atarudi nyumbani akiwa ni bingwa.” Aliongeza Guardiola ambaye pia staa wake mwingine, Leroy Sane alichaguliwa kuwa mwanasoka bora chipukizi wa msimu huu. Salah mpaka sasa amefunga mabao 31 na anaongoza kwa kufunga mabao katika Ligi Kuu ya England huku kwa ujumla akiwa amefunga mabao 41 katika michuano mbalimbali ikiwa ni msimu wake wa kwanza tangu anunuliwe na Liverpool akitokea Roma kwa dau la pauni 37 milioni katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Kwa kufanya hivyo, Salah anakuwa mchezaji wa saba wa Liverpool kutwaa tuzo hiyo huku mchezaji wa mwisho wa majogoo hao wa Anfield kuchukua tuzo hiyo akiwa ni staa wa Uruguay, Luis Suarez aliyechukua mwaka 2014.

Salah anapewa nafasi kubwa ya kuchukua kiatu cha dhahabu msimu huu mbele ya mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane, lakini mwenyewe amedai kwamba kwa sasa mawazo yake ameyaelekeza katika pambano la leo la nusu fainali dhidi ya Roma.

“Ni heshima kubwa. Nimefanya kazi ngumu na nina furaha kushinda tuzo hii. Nadhani haitakuwa ya mwisho. Najivunia kushinda na nimefanya kazi kubwa sana.” Alisema Salah ambaye anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka taifa la Misri kutwaa tuzo hizo.

“Ni heshima kuwa mchezaji bora wa mwaka katika Ligi Kuu ya England hususani ukiziangatia kwamba nimepigiwa kura na wachezaji wenzangu. Ninadhani kutoka katika siku ya kwanza nilipoondoka Ligi Kuu ya England ilikuwa katika akili yangu kupata mafanikio hapa. Sikupata nafasi Chelsea kwahiyo ilikuwa wazi katika akili yangu kwamba ningerudi siku moja. Nadhani niliondoka na nimerudi mtu tofauti, mwanaume tofauti na mchezaji tofauti.” Aliongeza Salah.