PSG yatupa ndoano kwa Zidane

Muktasari:

PSG ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa kwa mara ya mwisho mwaka 1995

Paris, Ufaransa. Paris Saint-Germain wameanza mazungumzo na Zinedine Zidane ili achukue jukumu la kuinoa timu hiyo, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari.
Miamba hiyo ya Ufaransa wanajiandaa na maisha nje ya Unai Emery hasa kama watashindwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Kibarua cha Emery kimekuwa shakani tangu kikosi chake kilipokosa ubingwa msimu uliopita uliokwenda kwa Monaco.
Usajili wa Neymar na Kylian Mbappe umewasaidia kurudi kileleni mwa ligi, lakini inaaminika bado mambo hayajatulia ndani ya kikosi hicho.
PSG ina malengo makubwa ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa na wanataka kumsajili kocha atakayewezesha klabu hiyo kufikia ndoto hiyo.
PSG itawakaribisha Real Madrid katika mchezo wa raundi 16 bora ya Ligi ya Mabingwa kipindi ambacho makocha wote wawili wa timu hizo wakiwa katika presha kubwa.
Zidane, ambaye ametwaa mara mbili mfululizo taji la Ligi ya Mabingwa amejikuta katika wakati mgumu ndani ya Bernabeu kutokana na timu hiyo kufanya vibaya katika La Liga.
Madrid kwa sasa ipo nafasi ya nne ikiwa nyuma kwa pointi 19 kwa mahasimu wao na vinara wa ligi hiyo Barcelona.