Mshahara wamponza Rooney kupata timu mpya ya kumsajili msimu huu

Muktasari:

Rooney ambaye ameshindwa kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kocha Jose Mourinho amekuwa akitaka kuihama klabu hiyo.

Manchester, England. Ndoto ya nahodha wa Manchester United, Wayne Rooney kupata timu mpya ya kuchezea msimu ujao imeingia doa baada ya klabu mbalimbali kutishwa na ukubwa mshahara wake.

Rooney ambaye ameshindwa kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kocha Jose Mourinho amekuwa akitaka kuihama klabu hiyo.

Lakini, mshahara wake wa Pauni 300,000 kwa wiki unazifanya klabu nyingi ziogope kuzungumza naye.

Kwa sababu hiyo, Rooney amekwama kwenye klabu hiyo ya Old Trafford  baada ya kukosa mahali ambako atauzwa kwa bei ndogo kuliko inayotakiwa na Manchester United.

Hadi sasa, Rooney, 31,  ana mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wake, anasubiri huruma ya United kupunguza bei ili kumwezesha kupata mahali pa kwenda. Kinyume chake, atabaki Old  Trafford bila kucheza na kuondoka akiwa mchezaji huru.

Klabu ya Everton  chini ya kocha  Ronald Koeman imekuwa ikimfuatilia mshambuliaji huyo aliyekulia Goodison Park.