Mpenzi wa Ronaldo ashuhudia Morocco ikizamishwa

Muktasari:

  • Kiwango bora katika dakika zote 90 za mchezo kilichoonyeshwa na Morocco dhidi ya Ureno jana hakikutosha kuwaokoa wawakilishi hao wa Afrika mbele ya aibu ya kuaga mashindano hayo kufuatia kipigo cha bao 1-0 ambacho walikipata kwenye mchezo huo.

Moscow, Russia. Imewachukua Morocco saa 19 tu kuendeleza majonzi ya Bara la Afrika yaliyoanzishwa na Misri kwenye Kombe la Dunia 2018 baada ya kuungana nao kuzipa mkono wa kwaheri fainali hizo.

Kiwango bora katika dakika zote 90 za mchezo kilichoonyeshwa na Morocco dhidi ya Ureno jana hakikutosha kuwaokoa wawakilishi hao wa Afrika mbele ya aibu ya kuaga mashindano hayo kufuatia kipigo cha bao 1-0 ambacho walikipata kwenye mchezo huo.

 

Bao la mapema lililofungwa na nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo jana sio tu liliyazima matumaini ya Morocco kutinga hatua ya pili ya mashindano hayo bali pia ilifanya Afrika iandike rekodi mbovu ya timu zake mbili mfululizo kuwa za kwanza kufungasha virago kwenye Kombe la Dunia mwaka huu.

Ronaldo alitumia muda wa dakika nne tu tangu filimbi ya kuanza mchezo ilipopulizwa, kufunga  bao hilo kwa kichwa cha kuchupa, ambalo lilizika rasmi matumaini ya Morocco kuingia hatua ya 16 Bora.

Bao hilo lilimaanisha kuwa Morocco watasubiri kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya Hispania kwa ajili ya kukamilisha ratiba na sio kusaka nafasi ya kucheza hatua ya pili ya michuano hiyo ya 16 bora.

Kipigo hicho cha jana kimewafanya wawakilishi hao wa Afrika kuaga fainali hizo kwani hata wakiibuka na ushindi kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Hispania, hawatoweza kufikia pointi za Ureno au mojawapo kati ya Iran au Hispania zilizocheza jana jioni.

Hata ikipata ushindi dhidi ya Hispania, Morocco itafikisha pointi tatu lakini matokeo yoyote ya mchezo baina ya Hispania yataiathiri na hivyo kuifanya iage rasmi mashindano hayo.

Kama Hispania itashinda, maana yake itafikisha pointi nne ambazo haziwezi kufikiwa na Morocco lakini pia hata ikifungwa, Iran itakuwa imefikisha pointi sita ambazo wawakilishi hao wa Afrika hawatoweza kuzifikia.

Na hata kama mechi baina ya Iran na Hispania ikimalizika kwa matokeo ya sare, maana yake Iran watafikisha pointi nne ambazo pia hazitoweza kufikiwa na Morocco.

Ikitambua kuwa inahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuweka hai matumaini ya kufuzu hatua inayofuata, Morocco ilionyesha kiu ya kusaka ushindi kwenye mchezo huo kwa kumiliki mpira muda mrefu wa mechi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Ureno lakini washambuliaji wake walikosa umakini wa kutumia nafasi walizotengeneza kuipa ushindi.

Wakati kipigo hicho kikizidi kupunguza wawakilishi wa Afrika kwenye Kombe la Dunia, upande wa pili kimeipa neema Ureno ambayo imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua zinazofuata.

Ikumbukwe kuwa kabla ya Morocco kutolewa mashindanoni, Misri ilikuwa ya kwanza kuaga baada ya kufungwa mabao 3-1 na Urusi, kipigo ambacho kilikuwa cha pili kufuatia kile cha bao 1-0 kutoka kwa Uruguay kwenye raundi ya kwanza.