Mourinho amuwinda nyota wa Croatia Ivan Perisic

Muktasari:

  • Mourinho amtetea winga huyo kwamba hakushika mpira makusudi kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Ufaransa juzi Jumapili na kumfanya mwamuzi Nester Pitana kuamuru ipigwe penalti baada ya kwenda kuangalizia picha za marudio ya tukio hilo kupitia VAR. Kauli ya Mourinho anaonekana kuguswa kabisa na kile kilichotokea dhidi ya mchezaji huyo anayemtaka aende kwenye timu yake.

JOSE Mourinho bana anapotaka lake, amekuwa mjanjamjanja sana. Si unafahamu kwa sasa anaifukuzia huduma ya winga wa Inter Milan na Croatia, Ivan Perisic, basi anachojaribu kufanya ni kumtetea na kumsifu staa huyo kila siku ili kumshawishi achague kwenda kujiunga na kikosi chake cha Manchester United huko Old Trafford.

Mourinho amtetea winga huyo kwamba hakushika mpira makusudi kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Ufaransa juzi Jumapili na kumfanya mwamuzi Nester Pitana kuamuru ipigwe penalti baada ya kwenda kuangalizia picha za marudio ya tukio hilo kupitia VAR. Kauli ya Mourinho anaonekana kuguswa kabisa na kile kilichotokea dhidi ya mchezaji huyo anayemtaka aende kwenye timu yake.

“Naunga mkopo mfumo huu wa VAR, lakini si kwa kile kilichofanyika kwenye fainali. Niliunga mkono mfumo huo nikiamini kwamba ungeondoa yale makosa makubwa kwenye soka, lakini si kutumika kwa ajili ya kutoa penalti tu na mengi haitumiki," alisema Mourinho.

“Imeonekana wazi kuna makosa. Hivi Perisic angerukaje juu na mkono wake ukiwa chini. Angewezaje kufanya hicho wanachosema wakati hatua chache mbele yake kulikuwa na mchezaji wa Ufaransa? Fainali si mechi ya kawaida, kufanya uamuzi ule wa VAR ulileta athari kubwa kwenye mechi.”

Kwenye dirisha lililopita, Perisic alifikia makubaliano binafsi kujiunga na Man United, lakini wababe hao wa Old Trafford walishindwa kukubaliana na Inter Milan kwenye ada ya uhamisho. Sasa Mourinho amepania kuinasa huduma yake hasa baada ya kutamba kwenye Kombe la Dunia 2018.