Mourinho ampagawisha Pogba kwa unahodha

Muktasari:

  • Manchester United imeanza Ligi Kuu kwa kishindo kwa ushindi

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amemtia ndimu kiungo wake Paul Pogba baada ya kumpa unahodha kwenye mchezo wa jana usiku wa ufunguzi wa Ligi Kuu England.

Katika mchezo huo Pogba alifunga bao la kwanza dakika ya tatu kwa mkwaju wa penalti, United ilipoifunga Leicester City kwa mabao 2-1 na kiungo huyo alikuwa kwenye kiwango cha juu sawa na kile alichokionyesha katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia.

Wachambuzi wa soka wanaamini kuwa Mourinho alitumia mbinu ya kumpa Pogba unahodha wa mchezo huo ili kumsukuma ajitume zaidi na hilo lilifanikiwa.

Mourinho ambaye msimu uliopita alimlaumu mchezaji huyo mara kadhaa akimtuhumu kucheza chini ya kiwango, aliamua kutumia mbinu hiyo, kjuzima ule msuguano uliokuwapo hasa ikizingatiwa Pogba aliomba kuihama United ili ajiunge na Barcelona.

Pogba ambaye alianza mazoezi na wenzake siku nne kabla ya mchezo huo, hivyo hakupaswa kucheza mchezo huo, lakini yeye mwenyewe akamuomba Kocha ampange na alicheza kwa kiwango cha juu sawa na alivyofanya kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Penalti ya kiufundi aliyoifunga akiupeleka mpira karibu na mwamba wa juu wakati kipa Kasper Schmeichel akianguka chini iliwainua vitii mashabiki wa United na penalti hiyo ilitokana na Daniel Amartey kuunawa mpira uliopigwa na Alexis Sanchez.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko, katika kipindi cha pili mlinzi wa pembeni kushoto Luke Shaw akaongeza la pili likiwa la kwanza kwake tangu apandishwe kucheza kikosi cha kwanza, alifunga kiustadi baada ya kupokea pande la Juan Mata.

Bao la kufutia machozi la Leicester lilifungwa na mtokea benchi Jamie Vardy kwa kichwa akiunganisha krosi ya Ricardo Perreira iliyogonga mwamba na kurudi uwanjani kisha mfungaji akauwahina kuukwamisha wavuni.

Tukio la kuvutia uwanjani lilikuja katika dakika za lala salama Leicester ilipopata kona na kipa Schmeichel aliliacha lango lake na kwenda mbele kusaidia kusaka bao la kusawazisha na nususra afunge bao lakini mpira aliopiga kichwa ulitoka sentimita chache.

Pogba alipumzishwa katika dakika ya 84 nafasi yake ikichukuliwa na Marouane Fellaini, huku Mourinho akijitetea kumchezesha kwa dakika nyingi licha ya kutofanya mazoezi ya kutosha.

"Tulipanga kumchezesha Pogba kwa angalau dakika 60 lakini akacheza zaidi ya dakika 80, kwa kuwa alionekana yupo fiti na alicheza kwa kiwango cha juu,” alisema Mourinho.