Mourinho Master Plan

Tuesday May 15 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND

MABOSI wa Manchester United wamemwambia Jose Mourinho, kutakuwa na Pauni 150 milioni za kufanya usajili wa mastaa wapya kwenye dirisha lijalo. Hapo sasa kazi ni kwake mwenyewe kama kwenda kusajili staa mmoja wa maana kwa pesa hiyo au kusajili staa zaidi ya mmoja, chaguo ni lake.

Lakini, Mourinho anafahamu wazi kupambana na Manchester City kwenye Ligi Kuu England msimu ujao itahitaji kuwa na wachezaji mahiri kwa kadiri inavyowezekana na ukitazama kikosi cha Man United, kinahitaji mastaa matata kuanzia wawili kwenda mbele.

Kutokana na hilo ndiyo maana kimekuwa kitu cha kawaida kusikia kwa kikosi hicho cha Old Trafford kuhusishwa na mastaa wenye majina makubwa kwenye soka kuanzia kwa Neymar, Antoine Griezmann, Gareth Bale, Paulo Dybala na hata Cristiano Ronaldo wakati mwingine.

Kwa kifupi tu, Mourinho anahitaji staa mwenye uwezo wa kuongeza kitu kwenye kikosi chake na kubadili matokeo inapohitajika kufanya hivyo.

Mourinho sasa ana mipango yake ya kuhakikisha anapata pesa ya kuongezea kwenye bajeti atakayopewa ili kuhakikisha anakuwa na uwezo wa kunyakua wachezaji anaowataka na kupunguza pia bili ya mishahara kwenye kikosi chake ili kuwa na kundi la wachezaji wachache watakaotumika kikamilifu.

Baadhi ya mastaa hawa safari ya kuondoka Old Trafford inaweza kuwahusu ili kupatikana kwa pesa na kutoa nafasi kwa wachezaji wengine maana kuja kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Anthony Martial

Hakuna ubishi, Mourinho anaweza kumhusisha Martial kwenye orodha ya wachezaji wanaopaswa kuondoka kwenye timu yake ili kuchangisha pesa itakayotosha kuongezea bajeti yake ya usajili ya Pauni 150 milioni. Martial amekuwa akilinganishwa na Thierry Henry na Kylian Mbappe, lakini ukweli ni kwamba ameshindwa kumpa ourinho kile ambacho anakitaka. Anaweza kudai hakupewa nafasi ya kutosha kufanya hivyo, lakini Mourinho kwa upande wake anaweza kusema Martial hakufanya inavyotosha kupata nafasi ambayo angepata. Juventus inahitaji saini yake na huenda akauzwa huko kwa ada isiyopungua Pauni 50 milioni.

Luke Shaw

Unajua Manchester United ndiyo timu iliyovuna pesa nyingi za malipo ya televisheni kwenye Ligi Kuu England kuliko mabingwa, Manchester City? Jambo hilo linawapa jeuri na kufikiria kufanya usajili mkubwa. Lakini, sambamba na hilo, kuna baadhi ya wachezaji ni lazima waondoke na mmoja wao ni beki wa kushoto Luke Shaw, iliyemsajili kutoka Southampton mwaka 2014.

Tangu alipotua Old Trafford, Shaw ameshindwa kuonyesha makali yake kuanzia wakati ule kikosi kilipokuwa chini ya Louis van Gaal hadi sasa kikiwa chini ya Mourinho. Ni jambo la wazi, Shaw ataondoka.

Paul Pogba

Tangu Alexis Sanchez alipotua kwenye kikosi cha Man United basi hapo yakaanza kuibuka matatizo ya Paul Pogba.

Kiungo huyo alidai anahitaji kupangwa upande wa kushoto, eneo ambalo Sanchez amekuwa bora zaidi. Jambo hilo liliibua matatizo mengi ikiwamo Pogba kuwekwa benchi na kuamsha maneno ya kwamba, ataondoka kwenye kikosi hicho. Mourinho hayupo tayari kuachana na Pogba, lakini kama Paris Saint-Germain inayoripotiwa kumtaka ikiweka pesa nyingi mezani, basi hakuna shaka mchezaji huyo atapigwa bei, ipatikane pesa ya kuongezea ili kumsajili Neymar.

David de Gea

Kwa mara kadhaa, Mourinho amekuwa akiweka ugumu uwezekano wa kipa wake namba moja kuondoka Old Trafford. Hata De Gea mwenyewe haonekani kuwa na mpango wa kulazimika kuhama.

Lakini, linapokuja suala la kutakiwa na Real Madrid kila kitu kinakuwa tofauti na huenda Man United ikashawishika kumpiga bei kipa huyo raia wa Hispania.

Kitu ambacho Man United inahitaji kwa sasa ni kuchangisha pesa kuongezea kwenye bajeti yake. Inaweza kuchukua uamuzi wa kumuuza kipa huyo kwa sababu kwenye kikosi wanaye Sergio Romero, ambaye pia ni matata kwelikweli anaposimama golini.

Marouane Fellaini

Kuna wakati alipokuwa mchezaji muhimu kwa Kocha Jose Mourinho hasa kabla ya ujio wa Nemanja Matic kwenye kikosi hicho.

Lakini, baada ya hapo, Fellaini amekuwa akicheza mechi mara moja moja sana kitendo kilichomfanya afikirie kuachana na timu hiyo hasa kwa kipindi kile ambacho timu za Uturuki na Inter Milan ya Italia zilionyesha dhamira ya kuhitaji huduma yake.

Kwa Fellaini, inachokisubiri Man United ni kupata tu mnunuzi na kama hilo likitokea basi itakubali kufanya biashara ili kuongezea bajeti yake ya usajili.

Matteo Darmian

Mambo yameshindwa kwenda vizuri kwa beki huyo Mtaliano. Kitu kinachoshangaza ni kumuona mchezaji huyo bado akiwa kikosini humo hadi sasa. Darmian kuna ofa zinazomhusu na ukweli ni kwamba kama kutakuwa na timu ambayo itakuwa tayari kutoa kiwango cha pesa ambacho wababe hao wa Old Trafford wanakihitaji, basi naye atakuwa kwenye orodha ya wachezaji watakaofunguliwa mpango wa kutoka ili kuja wengine ambao wataifanya Man United kuwa na nguvu mpya kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.

Daley Blind

Uzuri wa kuwa na huduma ya Daley Blind ni kwamba, ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti ndani ya uwanja. Lakini, ukweli mchezaji huyo atauzwa kwenye dirisha lijalo la usajili.

Blind amekuwa benchi kwa muda mrefu na jambo hilo limemfanya afikirie mpango wa kuhamia kwenye timu nyingine ili kupata nafasi ya kucheza na kwa Mourinho mambo yake yapo wazi kabisa.

Blind anahitaji kuondoa kwani anaonekana ni kati ya wachezaji wanaochukua tu mishahara mikubwa bila ya kutoa huduma inayostahili.