Mourinho: Kila mchezaji Man United anauzwa

MANCHESTER, ENGLAND

JOSE Mourinho amewachimba mkwara wachezaji wake kwenye kikosi cha Manchester United, akisema hakuna ambaye yupo salama kama tu dirisha la Januari litaendelea kuwa wazi.

Mreno huyo alisema amefungua milango ya kusikiliza ofa za timu yoyote itakayokuja kutaka mastaa wake na atakuwa tayari kufanya biashara kama itawekwa mezani ofa nzuri. Kauli hiyo ya Mourinho inawaweka mtegoni Henrikh Mkhitaryan na Marouane Fellaini, ambao ndiyo hakika maisha yao ndani ya Old Trafford yamekuwa kwenye shaka kubwa.

Mourinho kwa sasa anatolea macho mpango wa kusaini wachezaji wapya, akiwawinda mastaa wa Arsenal, Alexis Sanchez na Mesut Ozil na anamsaka pia beki wa kushoto wa Tottenham, Danny Rose na Ryan Sessegnon wa Fulham.

Lakini, kwenye kufanya hivyo Mourinho atalazimika kwanza kuwafungulia mlango wa kutokea baadhi wa mastaa wake ambao atawategemea wampe matokeo kwenye mechi ya leo Jumatatu dhidi ya Stoke City kwenye harakati zao za kuwafukuzia Manchester City ambao, jana Jumapili walikuwa na kibarua huko Anfield nyumbani kwa Liverpool.

Mourinho alisema: “Mtazamo wangu kwa wachezaji ni kila mchezaji ana bei yake. Haijalishi ni nani. Haijalishi kiwango. Haijalishi sifa wala hadhi yake. Nadhani kila mchezaji anayo bei yake. Mimi si kocha anayesema mchezaji huyu haguswi, huyu hawezi kuuzwa. Hivyo basi kama dirisha lipo wazi, basi yeyote anaweza kuuzwa kama kutakuwa na klabu itakayovutiwa na mchezaji wetu na ina ofa nzuri.”

Fellaini amegoma kusaini mkataba mpya na kiungo wa Ubelgiji akiwindwa na Besiktas, ambao wapo tayari kulipa Pauni 8 milioni. Wachezaji wengine ambao wapo kwenye hatihati ya kupigwa bei kwenye dirisha hili ni Luke Shaw, Matteo Darmian, Daley Blind, Anthony Martial, Ashley Young na Henrikh Mkhitaryan.