Mourinho: Hispania imebugi kwa Costa

JOSE Mourinho amesema Hispania imejitakia kutoka sare na Ureno kwenye mechi yao ya kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia na kosa lilianzia kwa Kocha Fernando Hierro kumtoa straika Diego Costa.

Straika huyo wa Atletico Madrid, Costa, aliyewahi kufanya kazi na Mourinho huko Chelsea, alifunga mara mbili kuisawazishia Hispania katika mechi hiyo na muda wote alikuwa msumbufu kwa mabeki wa Ureno hadi Hierro alipomtoa kwenye dakika ya 77 na kuharibu kila kitu.

Wakati huo, Hispania ilikuwa mbele kwa mabao 3-2, lakini baada ya kutoka mshambuliaji huyo, wachezaji wa safu ya ulinzi wa Ureno walianza kuondoka kwenye eneo lao kupeleka mipira mbele na kufanikiwa kufunga bao la kusawazisha liliwekwa wavuni na Cristiano Ronaldo kwa mpira wa adhabu.

“Nataka niseme, kwa upande wangu niliona mechi mbili, ile ambayo Diego Costa alikuwamo na ile aliyotolewa. Mechi ilibadilika sana baada ya kutolewa Costa.

Kwa mara ya kwanza mabeki wa Ureno walionekana kukaa nyuma bila ya kuja mbele, waliona wakiondoka na kuacha nafasi Costa atawaadhibu,” alisema Mourinho.

Costa amecheza mechi 21 kwenye kikosi cha Hispania na kufunga mabao tisa.