Mo Salah bado ni kitendawili kuikabili Uruguay

Wednesday June 13 2018

 

By Fadhili Athumani

Moscow, Russia. Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Misri, Hossam Mido, ana mashaka kama Salah, atarudi katika kiwango chake, kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Dunia 2018, inayotimua vumbi kesho.
Uwepo wa Salah katika mechi ya pili ya kundi A, kati ya Misri na Uruguay, itakayopigwa baada ya mchezo wa kukata utepe kati ya wenyeji Russia na Saudi Arabia, bado ni kitendawili, kwani inavyoonekana, jeraha la begani alilolipata, bado halijapona vizuri.
Kukosekana kwa Salah (25), ni pigo kubwa kwa kikosi cha Hector Cuper, ambao pia wana kibarua kigumu cha kukabiliana na wenyeji Russia na Saudi Arabia, katika hatua ya makundi.
Mido, ambaye aliifungia Misri mabao 20 katika mechi 51 alizoingia dimbani, anaamini kuwa Salah atapona haraka japo hana uhakika kama nyota huyo wa Liverpool atakuwa fiti kuwakabili Uruguay.
"Wamisri wanamuombea, kila mtu anajivunia kipaji cha Salah, hofu yetu ni utayari wake kabla ya mechi ya kwanza. Tunatamani awepo ila kwa sasa bado ni kitendawili kwa kweli," alisema Mido.
Salah alifunga mabao 44, katika msimu wake wa kwanza akiwa na shati la Liverpool kwenye EPL,  akashinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu na tuzo zingine kibao.