Miki amsubiri Emery, mastaa kibao kutua Arsenal

STAA wa Arsenal, Henrikh Mkhitaryan anaamini kocha mpya kwenye kikosi hicho atakuja kufanya mapinduzi ya kiufundi la kuifanya klabu hiyo kuwa tishio kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.

Arsenal ilimtangaza Unai Emery kuwa kocha wao mpya anayekuja kurithi mikoba ya Arsene Wenger, huku Mhispaniola huyo akibainisha mipango yake ya kuifanya timu hiyo kuwa ya ushindani na kupambana na timu ngumu kama Manchester City kwenye mbio za ubingwa msimu ujao.

Mkhitaryan alitua Emirates, Januari tu hapo kwenye dili lililomhusisha Alexis Sanchez kwenda Manchester United na hakuna ubishi staa huyo wa kimataifa wa Armenia, amehuzunika kwa Wenger kuondoka, lakini sasa anaamini chini ya Emery timu itafanya vizuri zaidi na kuwa na mipango tofauti.

“Namtumaini ataleta mbinu na mawazo mapya kwenye timu na tutafanikiwa,” alisema Mkhitaryan.

“Bado sijakutana naye, hatukupata muda wa kuzungumza na sijazungumza na wenzake pia kuhusu kocha huyo, hivyo itakuwa vyema kama nikikutana naye. Kila mtu hapa ni profesheno.”

Mipango ya Emey imefichuliwa ni kuleta mastaa wa maana kikosi, huku ikitajwa orodha ndefu ya wachezaji hao ambao baadhi yao sura zao zitakuwa kwenye uzi wa Arsenal msimu ujao. Wachezaji wanaohusishwa na Arsenal tangu Emery alipotangazwa kuchukua mikoba ya Wenger ni pamoja na Ever Banega, Jean-Michael Seri, Ivan Rakitic, Adrien Rabiot, Anthony Martial, Sokratis Papastathopoulous, Steven N’Zonzi, Bernd Leno na Ousmane Dembele.