Messi atua Russia akiidharau England

Tuesday June 12 2018

 

LIONEL Messi ameongea kitu ambacho Waingereza hawatapenda kukisikia. Keshokutwa Alhamisi Kombe la Dunia litaanza pale Russia, lakini Waingereza wakitafakari kauli ya Messi kuelekea katika michuano hiyo itawatumbukia nyongo.

Messi ambaye hajawahi kutwaa taji hilo la Kombe la Dunia licha ya kutwaa mataji mbalimbali duniani, amezitaja timu sita ambazo zinaweza kuchukua taji hilo lakini akawaweka kando Waingereza ambao wanasaka taji lao la kwanza la michuano hiyo tangu mwaka 1966.

“Kuna timu kadhaa ambazo zitakwenda katika fainali hizi zikiwa zinajiamini, zinacheza vizuri na zina wachezaji mmoja mmoja ambao ni wazuri. Timu hizo ni kama Brazil, Ujerumani, Hispania, Ufaransa na Ubelgiji. Ingawa Ubelgiji haitajwi sana,” alisema Messi.

“Argentina ina wachezaji wazuri na uzoefu wa fainali zilizopita za Kombe la Dunia itasaidia. Itakuwa michuano ambayo timu zinalingana nguvu,” alisema Messi bila ya kuitaja England ambayo mara zote imekuwa ikijipa matumaini makubwa kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.

Hii inaweza kuwa michuano ya mwisho kwa Messi baada ya kushindwa kulitwaa taji hilo mara nne (2006, 2010, 2014) huku pia akishindwa kulitwaa taji la Marekani ya Kusini ambalo amefika fainali tatu tofauti.

Argentina ambayo imetwaa taji la Kombe la Dunia mara mbili (1978 na 1986) imekuwa na kiu kubwa ya mafanikio kutokana na vipaji lukuki katika nchi hiyo, lakini mambo yamekuwa tofauti. Taji lake la mwisho kuchukua ilikuwa mwaka 1993 wakati ilipochukua Copa America.

Kimtazamo, Argentina imepawa kundi jepesi baada ya kuhangaika kufuzu katika michuano yenyewe. Imepangwa na Iceland, Nigeria na Croatia na inatazamiwa kuibuka viongozi wa kundi hilo.

Mshindi wa kundi hilo D anatazamiwa kucheza na mshindi wa pili wa Kundi C ambalo lina nchi za Ufaransa, Australia, Peru na Denmark. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ambaye atakuwa mchambuzi huko Russia, anaamini Argentina ina nafasi ya kucheza na Australia aliyoitabiria kushika nafasi ya pili katika Kundi C.

Messi ambaye anatazamiwa kutimiza umri wa miaka 31 wakati fainali hizo zikiendelea Russia, amedokeza anaweza asistaafu baada ya kumalizika kwa michuano hiyo baada ya kuulizwa atachukua uamuzi gani kama Argentina ikichukua michuano hiyo.

“Nimetwaa mataji mengi na klabu na mara nyingi mwaka unaofuata bado ninakuwa na kiu ile ile ya mafanikio.

“Mara zote wazo langu linakuwa kushinda tena. Kwa Kombe la Dunia itakuwa hivyo hivyo. Sitabadilika,” alisema Messi.

Argentina inatazamiwa kucheza mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Iceland Jumamosi kabla ya kucheza mechi yake ya pili dhidi ya Croatia Alhamisi ya Juni 21 na kisha kumalizia mechi ya makundi kwa kucheza na wababe wa Afrika, Nigeria Juni 26. Katika fainali za Kombe la Dunia zilizopita Argentina ilifika fainali, lakini ikajikuta ikichapwa bao 1-0 na Ujerumani katika pambano lililochezwa uwanja mkubwa wa Brazil, Maracana.

Bao pekee la Ujerumani katika fainali hizo lilifungwa na kiungo, Mario Gotze ambaye hata hivyo, mwaka huu ameachwa nje ya kikosi hicho.

Mara zote mafanikio ya Messi katika kiasi cha kuitwa mchezaji bora wa muda wote duniani, yamekuwa yakikwama kutokana na kushindwa kutwaa Kombe la Dunia ambalo wakali wa zamani wanaolinganishwa naye kama Pele na Diego Maradona wamekuwa wakiheshimika zaidi kwa kulitwaa taji hilo katika nyakati tofauti.