Konta achemka kufuzu mashindano ya tenisi

Muktasari:

Konta anayetajwa mmoja wa wachezaji warembo wa tenisi kama ilivyo kwa Maria Sharapova au Serena Williams, alikuwa akipewa nafasi ya kushiriki fainali hizo wiki ijayo, lakini amelazimika kujiengua kutokana na maumivu ya mguu.

London, England. Kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya tenisi, Anna Keothavong amesema ameshtushwa na kitendo cha mchezaji Jo Konta, kushindwa kufuzu katika fainali za WTA mjini Singapore.
Konta anayetajwa mmoja wa wachezaji warembo wa tenisi kama ilivyo kwa Maria Sharapova au Serena Williams, alikuwa akipewa nafasi ya kushiriki fainali hizo wiki ijayo, lakini amelazimika kujiengua kutokana na maumivu ya mguu.

Hata hivyo, kocha huyo anaamini mchezaji huyo atarejea akiwa na kiwango bora katika michuano ya mwakani. Konta anashika nafasi ya kwanza kwa ubora England na duniani nafasi ya nne.

Mchezaji huyo alikuwa kwenye kiwango bora katika michuano ya US Open akiwa miongoni mwa wachezaji wanane wanawake waliokuwa wakipewa nafasi ya kutwaa ubingwa kabla ya wiki hii kuachana na kocha wake Wim Fissette.
“Nimeshtushwa na tukio hili kwa sababu hii ni mara ya pili kwake kujitoa katika michuano akiwa katika ubora wake. Nimehuzunishwa sana kwanini matatizo haya yanampata yeye tu,” alisema kocha huyo.