Mashabiki wamchenjia Ronaldo

MADRID,  HISPANIA

KWELI ukichoka, watu wanakuchoka zaidi. Cristiano Ronaldo kachoka na mashabiki wake huko Real Madrid wamemchoka zaidi.

Baada ya staa huyo kushuhudia kikosi chao kikichapwa na Villarreal na kupoteza matumaini kabisa ya kuikamata Barcelona kwenye mbio za ubingwa wa La Liga, mashabiki wa timu hiyo wameamua kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kurusha maneno makali kwa staa huyo wa Ureno.

Kuna mashabiki waliofika mbali wakisema Ronaldo amekwisha kutokana na kushindwa kufanya kitu cha maana kuibeba timu yake kupata matokeo ya ndani ya uwanja. Katika mchezo huo, kikosi hicho cha Zinedine Zidane kilichapwa 1-0, shukrani kwa bao la dakika 87 la Pablo Fornals, ambalo limewatia aibu mbele ya mashabiki wao lukuki huko Bernabeu.

Matokeo hayo yameifanya Real Madrid sasa kuwa nyuma kwa pointi 16 dhidi ya vinara Barcelona kwenye msimamo wa La Liga kabla ya mechi za jana.

Sasa mambo yamemgeukia Zidane, licha ya kusaini mkataba mpya miaka miwili iliyopita, kinachojadiliwa kwa sasa ni kuhusu hatima yake katika timu hiyo kutokana na mwendo wa kusuasua kwenye ligi.

Ronaldo, mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or alipoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga na hilo ndilo lililowatibua mashabiki wa timu hiyo na kumrushia maneno makali wakisema amekwisha, hana jipya tena ndani ya kikosini chao kwa sasa.