Mashabiki Arsenal wasubiri usajili wa N'Golo Kante

Wednesday July 11 2018

 

LONDON, ENGLAND. UNAI Emery anashusha tu kichwa kimoja baada ya kingine. Tayari ameshadondosha mastaa watano wapya kwenye kikosi chao akiwamo kiungo mkata umeme, Lucas Torreira.

Emery amewafanya mashabiki wa Arsenal kupagawa kwamba sasa wamempata N'Golo Kante wao baada ya kumshuhudia Torreira kile alichokuwa akikifanya kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia akiwa na kikosi cha Uruguay.

Sasa msimu ujao kwenye Ligi Kuu England, Torreira utamwona ndani ya uzi wa Arsenal kila wiki. Mastaa wengine walionaswa na Emery hadi sasa kwenye kikodi hicho ni pamoja na kiungo Matteo Guendouzi, kipa Bernd Leno na beki wa kati Sokratis Papastathopoulos na beki wa kulia, Stephan Lichtsteiner. Torreira atavaa jezi namba 11 kwa msimu ujao.

“Huyu Lucas Torreira, tumesajili mchezaji kijana mwenye kipaji matata kabisa kwenye soka,” alisema Emery.

“Ni kiungo mwenye ubora usio na mashaka, binafsi nilifurahia sana nilipokuwa nikimwona akicheza kule Sampdoria kwa misimu miwili iliyopita na tumeona alivyofanya vyema na Uruguay kwenye Kombe la Dunia. Tunamkaribisha Lucas kwenye chama la Arsenal.”