Mandawa ashangaa kuachwa Stars

Muktasari:

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Mandawa katika Ligi Kuu Botswana amecheza michezo 9, na kufunga mabao matatu hadi sasa.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na BDF XI ya Botswana, Rashid Mandawa amesema bado anaimani ya kuitwaa kuichezea Taifa Stars.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Mandawa katika Ligi Kuu Botswana amecheza michezo 9, na kufunga mabao matatu hadi sasa.
Leo saa 10:00 jioni Mandawa ataiongoza BDF XI kucheza mechi ya ligi dhidi ya UF Santos.
Mandawa tangu alipoondoka nchini mwanzoni mwa mwaka huu akitokea Mtibwa Sugar hajapata nafasi ya kuichezea Stars inayonolewa na Salum Mayanga.
Kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitaingia kambini wiki ijayo kujiandaa na mashindano ya Chalenji, lakini jina la mshambuliaji huyo anayefanya vizuri Botswana likikosekana.
Kocha Kili Stars, Ammy Ninje ametangaza kikosi chake kitakachokuwa na washambuliaji Mbaraka Yusuph wa Azam,Yohana Mkomola wa Étoile Sportive du Sahel ya Tunisia na Daniel Lyanga wa Fanja na Elias Maguli wa Dhofar za Oman.