Manchester City yamweka sokoni Stones

Muktasari:

Kocha wa Man City Pep Guardiola amemwambia beki huyo wa kimataifa wa England kujiandaa kuondoka majira ya kiangazi.

LONDON, ENGLAND. MANCHESTER City imemweka sokoni beki wa kati John Stones baada ya kushindwa kucheza kwa kiwango bora.

Kocha wa Man City Pep Guardiola amemwambia beki huyo wa kimataifa wa England kujiandaa kuondoka majira ya kiangazi.

Guardiola amemnunua kwa bei mbaya Stones kutoka Everton muda mfupi baada ya kutua Man City kutoka Bayern Munich.

Stones amepoteza namba katika kikosi cha kwanza na kuwa beki chaguo la nne baada ya Man City kumsajili Aymeric Laporte katika dirisha dogo Januari, mwaka huu.

Stones anadaiwa kushindwa kuziba vyema pengo la nahodha wake Vincent Kompany aliyekuwa majeruhi muda mrefu.

Guardiola amekuwa akiwatumia mabeki Nicolas Otamendi na Laporte katika mashindano mbalimbali msimu huu.

Stones hakuwahi kuanza mchezo wa Ligi Kuu England tangu Januari baada ya kupata majeraha ya misuli.

Hata hivyo kocha wa England Gareth Southgate anatarajiwa kumtumia Stones katika kikosi cha kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Russia.