Man United yapata pigo

Saturday November 11 2017

 

London, England. Manchester United imeendelea kupata pigo, baada ya idadi ya wachezaji wake majeruhi kuongezeka.
Beki wa timu hiyo Phil Jones alitoka kwa msaada wa madaktari, baada ya kupata maumivu ya mguu katika mchezo wa juzi usiku.
Jones alipata maumivu katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki ambao England ilitoka suluhu na Ujerumani.
Bila shaka hilo ni pigo kwa kocha Jose Mourinho anayembana na majirani zake Manchester City kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Mourinho amekuwa akilalama kuhusu idadi kubwa ya majeruhi inayoyotishia kutibua ndoto yake ya kutwaa ubingwa wa England.
Beki huyo alianza kuchechemea dakika ya 10, lakini aliendelea kupambana hadi dakika ya 24 ambapo alilazimika kutoka na paja la mguu wa kushoto ulifungwa bandeji.
Jones, mmoja wa mabeki tegemeo Man United alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuokoa bao katika mstari kufuatia shuti la Leroy Sane.
Kocha wa England Gareth Southgate, alifanya uamuzi wa haraka kumbadili mchezaji huyo.
Mourinho anaweza kuibua mzozo na Southgate kwa kumtumia Jones akiwa na maumivu ya paja.
Beki huyo wa kati alicheza akiwa na bandeji katika paja la mguu wa kushoto hatua inayoweza kumpa nafasi Mourinho kulalamika kwa Chama cha Soka (FA).