Man United leo, Chelsea itakuja kesho

Muktasari:

Lakini, achana na hilo la kesho. Hii leo Jumanne, kocha wa Manchester United, Jose Mourinho hajielewi ama ampange Paul Pogba au asimpange katika mechi yao ya marudiano dhidi ya Sevilla kwenye mchakamchaka huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayofanyika huko Old Trafford.

Manchester, England. Mshambuliaji Olivier Giroud amesema hivi, Chelsea ina viwango vyote vya kuichapa Barcelona kwao Nou Camp na kuwatupa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu wakati timu hizo zitakapomenyana kesho Jumatano.
Lakini, achana na hilo la kesho. Hii leo Jumanne, kocha wa Manchester United, Jose Mourinho hajielewi ama ampange Paul Pogba au asimpange katika mechi yao ya marudiano dhidi ya Sevilla kwenye mchakamchaka huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayofanyika huko Old Trafford.
Pogba hakucheza mechi ya Jumamosi dhidi ya Liverpool, ambapo Mourinho aliwatumia viungo Scott McTominay, Nemanja Matic na Juan Mata. Man United itahitaji kushinda mchezo huo ili kufuzu hatua ya robo fainali baada ya mechi iliyopita kumalizika kwa sare ya bila kufungana huko Seville, Hispania. Sare yoyote ya mabao itakuwa na faida kwa Sevilla.
Giroud pia anaamini Chelsea walishindwa kuwachapa Barcelona kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika Stamford Bridge baada ya kutoka sare ya 1-1, lakini watakakwenda kufanya kweli Nou Camp.
Mechi nyingine za hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zitakazopigwa wiki hii, AS Roma itakuwa nyumbani kuwakaribisha Shakhtar Donetsk leo, wakati kesho, itakuwa zamu ya Besiktas watakaokuwa nyumbani kucheza na wababe wa Ujerumani, Bayern Munich.
Timu nne ambazo tayari zimeshatinga hatua ya robo fainali hadi sasa ni Real Madrid, Juventus, Liverpool na Manchester City.