Man City ni hatari

Muktasari:

Kabla ya ushindi wa juzi, City iliichapa Watford 6-0 ikiwa ugenini na kabla ya hapo walikuwa wameitandika Liverpool 4-0 katika Uwanja wa Etihad na hivyo kuwa moja kati ya timu tishio zaidi katika ufungaji msimu huu.

MANCHESTER  ENGLAND

KIMYA kimya, Manchester City na kocha wake, Pep Guardiola inaonekana kumfukuza mwizi bila ya kelele. Sasa imetangaza hali ya hatari kwa klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu England msimu huu.

Juzi City iliichapa Crystal Palace 5-0 katika dimba la Etihad na kwa kufanya hivyo inakuwa imefunga mabao 16 katika mechi tatu tu zilizopita Ligi Kuu England huku wavu wake ukiwa haujaguswa katika mechi hizo ilizofanya sherehe ya mabao.

Kabla ya ushindi wa juzi, City iliichapa Watford 6-0 ikiwa ugenini na kabla ya hapo walikuwa wameitandika Liverpool 4-0 katika Uwanja wa Etihad na hivyo kuwa moja kati ya timu tishio zaidi katika ufungaji msimu huu.

Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya City iliichapa Feyenoord ya Uholanzi mabao 4-0 ugenini lakini ni katika Ligi Kuu England ndipo City inaonekana kuwaogopesha mashabiki wa klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu England.

Kwa ushindi wa juzi, City inakuwa timu ya kwanza Ligi Kuu England kushinda mabao matano au zaidi ndani ya mechi tatu mfululizo ndani ya msimu mmoja, mara ya mwisho ikiwa imefanywa hivyo na Blackburn msimu wa 1958-59.

City pia imeonyesha uhodari katika kupiga pasi nyingi uwanjani ikiwa ni staili ya kocha wao wa sasa Guardiola na bao la tano lililofungwa juzi na kiungo, Fabian Delph lilitokana na pasi 31 za wachezaji wa City.

Bao hilo ndilo lenye pasi nyingi zaidi kabla ya kufungwa tangu Septemba 2015 na wachezaji 10 wa City wote waligusa mpira kabla ya Delph ambaye ni nyota wa England kumalizia kwa bao maridadi lililofunga mchezo wa juzi.

Kuashiria City haifungi mabao kwa kubahatisha, mpaka sasa kiungo wao mahiri mchezeshaji wa timu ya taifa ya Hispania, David Silva anaongoza kwa kupiga basi nyingi za mwisho za mabao Ligi Kuu England ambapo amepiga pasi sita za mabao.

Kiwango cha City pia kimerudisha uwezo wa mastaa wake wengi ambapo winga, Raheem Sterling aliyekuwa anahusishwa kwenda Arsenal tayari amefunga mabao matano katika mechi nne zilizopita. Awali alitumia mechi 31 kufunga mabao matano msimu uliopita.  Winga wa kimataifa wa Ujerumani, Leroy Sane naye anaonekana kuwa moto na hashikiki. Sane amefunga mabao matano katika mashuti sita tu aliyopiga yakalenga lango msimu huu wa michuano mbalimbali na kila kukicha kiwango chake kinaonekana kuwa moto.

Kama vile haitoshi, baadhi ya mastaa wa City wanajiandaa kuanza kuvunja rekodi mbalimbali za mastaa wa zamani wa Manchester City. Mmoja wapo ni mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Sergio Aguero ambaye kwa kufunga bao moja juzi anabakisha bao moja tu kuwa mfungaji bora wa muda wote Manchester City.

Aguero alifunga bao moja dhidi ya Palace na hivyo kufikisha idadi ya mabao 176 na endapo atafunga bao jingine katika mechi yoyote inayofuata ya City basi ataifikia rekodi ya mshambuliaji, Eric Brook ambaye alifunga mabao 177 miaka 78 iliyopita.

City wanatazamiwa kurudi uwanjani kesho usiku katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Shaktar Donetsk na wikiendi ijayo watazamiwa kutua katika uwanja mgumu wa Stamford Bridge kupambana na watoto wa Kocha Antonio Conte Chelsea katika pambano linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa Ligi Kuu England.