KIMEWAKA: Man City imeshinda tena, Arsenal yachomoa usiku

LONDON, ENGLAND

MANCESTER City mwaka wa raha. Ndiyo unachoweza kusema baada ya kuendeleza moto wake wa ushindi ikishinda mechi ya 15 kwenye Ligi Kuu England msimu huu baada ya kuwachapa Manchester United 2-1 kwao uwanjani Old Trafford.

Mabao mawili yaliyoanzia kwa mipira ya adhabu, ambayo iliwafanya Man United kushindwa kuokoa iliwakuta kwenye njia wachezaji David Silva na Nicolas Otamendi yalitosha kwa Man City kufunga mabao muhimu kabisa kwenye mechi hiyo na kufanikiwa kuweka pengo la pointi 11 dhidi ya Man United kwenye mchakamchaka wa mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Man United ilifunga bao lake kupitia kwa Marcus Rashford. Ushindi wa Man City kwa mechi hiyo ya jana Jumapili umewafanya kufikisha pointi 46, huku wakivunja rekodi yao kwa kuwa timu ya kwanza kuifunga Man United uwanjani Old Trafford tangu Septemba 10, 2016. Mabao ya Man City kwa mchezo huo wa jana imeonekana wazi kabisa ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu England unawataka wababe hao wanaonolewa na Pep Guardiola. Man City bado haijapoteza mechi msimu huu, ikishinda 15 na kutoa sare mara moja katika mechi 16 ilizocheza.

Katika mechi nyingine iliyopigwa jana, Olivier Giroud alitumia dakika 16 tu ndani ya uwanja kuiokoa Arsenal kutoka kwenye kipigo baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema sana la Southampton katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika kwenye Uwanja wa St Mary’s jana Jumapili. Charlie Austin alifunga dakika ya tatu tu ya mchezo, bao ambalo liliwatoa kijasho mastaa wa Arsenal akiwamo Mesut Ozil, Alexis Sanchez na Alexandre Lacazette kulirudisha hadi hapo alipoingia mwana asiyekubalika sana huko Emirates, Giroud kuja kuokoa jahazi kwa kusawazisha kwa kichwa katika dakika ya 88, kukifanya kikosi hicho cha Arsene Wenger kuondoka kwenye uwanja wa ugenini na pointi moja kufuatia sare ya 1-1.

Giroud aliingia dakika 72 kuchukua nafasi ya Lacazette na dakika 16 baadaye aliunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Sanchez katika dakika ya 88 na kuifanya walau Arsenal kuambulia pointi moja inayowafanya wafikishe pointi 29, ambazo bado zinawanyima nafasi ya kuingia ndani  ya Top Four. Kwa namna ambavyo Arsenal ilicheza mechi ya jana ni jambo gumu kuamini kama Alhamisi iliyopita tu hapo, ilishusha kipigo kizito kwa BATE Borisov kwa kuwachapa Bao Tano Bila kwenye Europa League. Hata hivyo sare hiyo kwa Arsenal ni bahati tu kuipata baada ya Southampton kupoteza nafasi kadhaa ambazo kimsingi zingeweza kuleta mabao mengi kwa upande wao baada ya mabeki wa Arsenal kuonekana kufanya makosa mechi kweli kwenye mechi hiyo.

Mabeki wa Arsenal wanaonekana kutokuwa fiti siku za karibuni, wakipoteza mipira mara nyingi sana katika eneo lao jambo ambalo liliwagharimu Jumamosi iliyopita wakati walipochapwa 3-1 na Manchester United kwenye Uwanja wa Emirates. Katika mechi 16 ilizocheza Arsenal kwa msimu huu, imeshinda mara tisa, sare mbili na vichapo vitano ambavyo zinafanya wawe wamekusanya pointi 29, huku wakiwa wamefunga mabao 30 na kufungwa 20.

Katika mchezo mwingine, Mohamed Salah ameendeleza moto wake wa kutupia baada ya kuifungia bao Liverpool, lakini safari hii mambo hayakwenda vizuri baada ya Everton kuchomoa kwa mkwaju wa penalti ya Wayne Rooney huko Anfield. Matokeo hayo yanaifanya Liverpool kufikisha pointi 30 na hivyo kuendelea kubaki kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu, wakishindwa kuiporomosha Chelsea baada ya kipigo chao cha juzi Jumamosi mbele ya West Ham United. Salah sasa ametupia mabao 13 kwenye ligi hiyo na kuwa kinara wa mabao.