MIKONO HEWANI: Wanyama apigiwa saluti Uingereza

10 mil Kiasi cha Pauni ambacho Wanyama alinunuliwa na Tottenham akitokea Southampton

London ENGLAND. UNATAKA uondokane na majanga? Basi muigie Victor Wanyama wa Tottenham anavyocheza. Ndiyo ushauri aliopewa kiungo wa Arsenal, Granit Xhaka, ambaye kwa sasa yupo katika majanga makubwa ya kadi nyekundu za mara kwa mara.

Mshambuliaji staa wa zamani wa Arsenal, Ian Wright ambaye kwa sasa ni mchambuzi mashuhuri wa soka nchini Uingereza, amemtaka kiungo huyo wa Arsenal kuiga uchezaji wa Wanyama kama anataka kuondokana na kadi zisizo na sababu.

Xhaka, ambaye ni nyota wa kimataifa wa Uswisi alipewa kadi nyekundu katika pambano dhidi ya Burnley Jumapili iliyopita na nusura aigharimu timu yake hiyo iliyoshinda mechi hiyo 2-1 kwa bao la penalti ya dakika ya majeruhi iliyofungwa na Alexis Sanchez.

Wright amemsifu Wanyama, ambaye ni kiungo wa kimataifa wa Kenya kwa jinsi anavyoulinda ukuta wake huku akiwa hachezi rafu tena kama ilivyokuwa wakati akiwa na Southampton msimu mmoja uliopita na amemtaka Xhaka afuate nyayo.

“Unapowatazama wachezaji wenye nguvu, tazama kiwango cha Wanyama wa Tottenham kwa sasa. Haumwoni akicheza rafu hizo na anaonekana kumiliki kila kitu.

Anachukua mpira, anauachia kwa urahisi na anafanya hii kazi mbele ya ukuta wake wa mabeki wanne,” alisema Wright.

“Ni matumaini yetu kwamba Xhaka ataimarisha mchezo wake kwa sababu anahitajika kufanya hivyo,” alisema Wight ambaye ameendelea kuwa shabiki wa timu yake ya Arsenal baada ya kustaafu.

Awali akiwa na Southampton, Wanyama alikuwa akisifika kwa kucheza soka la nguvu na lenye rafu nyingi, ambapo msimu uliopita alipewa kadi nyekundu tatu huku akipokea nne za njano. Hata hivyo, msimu huu chini ya kocha wake wa zamani wa Southampton, Mauricio Pochettino bado hajapewa kadi nyekundu mpaka sasa.

Wanyama aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 10 milioni na Tottenham, ameongeza nguvu katika safu ya kiungo ya Spurs na wakati ikitegemewa kuwa angeweza kuwekwa benchi na kiungo wa timu ya taifa ya England, Eric Dier, yeye ndiye ameibuka kuwa mchezaji muhimu zaidi katika eneo hilo.

Wanyama amecheza mechi zote 22 za Tottenham msimu huu na kwa sasa anaibeba timu hiyo baada ya kuumia kwa mlinzi wao mahiri wa kati, Jan Vertonghen ambapo, Wanyama alirudishwa kucheza beki wa kati katika pambano dhidi ya Manchester City.

Kwa upande wa Xhaka, licha ya kupewa kadi nyekundu mbili msimu huu tayari ana kadi tatu za njano, kitu ambacho sio rekodi mbovu sana, lakini tayari amesababisha penalti mbili kitu ambacho kinatia shaka katika nidhamu yake ya mchezo.

Kuanzia April 2014 Xhaka amepewa kadi tisa nyekundu akiwa na timu yake ya zamani Borussia Monchengladbach, Arsenal pamoja na timu yake ya taifa ya Uswisi.

Kuanzia mwanzo wa msimu uliopita mpaka leo, Xhaka amepewa kadi tano nyekundu akiwa mchezaji aliyepewa kadi nyingi zaidi katika Ligi Kubwa tano za Ulaya ambazo ni England, Hispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa.

Hata hivyo, Xhaka aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 30 milioni bado anapewa nafasi ya kufanya makubwa katika siku za usoni kama akitulia ambapo, ameonekana kuwa hodari katika kukaba, kusambaza mipira na kupiga mashuti makali kulenga lango la wapinzani hivyo, ni suala la kusbiri kuona.