Liverpool yatia hofu wapinzani wake

Muktasari:

Liverpool ambayo mara ya mwisho kuuchukua ubingwa huo ilikuwa miaka 28 iliyopita, imefanikiwa kumnasa kipa huyo kutoka AS Roma kwa dau la Pauni 67 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia kwa upande wa makipa.

LONDON, ENGLAND. WANAMKIMBIZA mwizi kimya kimya. Baada ya kufanikiwa kumnasa kipa wa kimataifa wa Brazil, Alisson Becker, kwa dau la uhamisho lililoweka rekodi ya dunia, Liverpool sasa inawekwa nafasi ya pili katika uwezekano wa kutwaa ubingwa wa England msimu ujao nyuma ya Manchester City.

Liverpool ambayo mara ya mwisho kuuchukua ubingwa huo ilikuwa miaka 28 iliyopita, imefanikiwa kumnasa kipa huyo kutoka AS Roma kwa dau la Pauni 67 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia kwa upande wa makipa.

Uamuzi huo unatokana na Kocha Jurgen Klopp, kutowaamini makipa wake wawili wa kwanza wa msimu uliopita, Simon Mignolet na Loris Karius ambaye alifanya makosa ya kijinga katika pambano la fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid mwezi Mei.

Jeuri ya Liverpool haitokani na kipa huyo tu, bali jinsi ambavyo Klopp ametatua tatizo la eneo la kiungo kwa kufanikiwa kuwanasa viungo watatu mahiri, Naby Keita, kutoka RB Leipzig, Fabinho kutoka Monaco na Xherdan Shaqiri kutoka Stoke City.

Matajiri wa Liverpool wametumia Pauni 170 milioni kwa ajili ya kutatua matatizo ya sehemu ya kiungo pamoja na kipa katika dirisha hili huku Januari wakiwa wametatua tatizo la ulinzi wa kati kwa kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia kwa eneo la ulinzi kwa kumchukua beki, Virgil Van Dijik, kwa dau la Pauni 75 milioni akitokea Southampton.

Kulikuwa na hofu huenda kuondoka kwa Philippe Coutinho katika dirisha la Januari pamoja na kuondoka kwa Emre Can kwenda Juventus katika dirisha hili kungeweza kudhoofisha eneo la kiungo la wababe hao wa Anfield, lakini habari imekuwa tofauti.

Liverpool pia imefanikiwa kuwabakiza mastaa wake watatu wa mbele; Roberto Firmino, Sadio Mane na Mohamed Salah, wasiende timu kubwa na watatu hao wamejenga ushirikiano wa kutisha katika safu ya ushambuliaji.

Wakati Mane alikuwa akitajwa kwenda Real Madrid kama Kocha Zinedine Zidane angeendelea kubakia klabu hapo, Salah ambaye alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu England na michuano yote msimu uliopita alikuwa pia akihusishwa kwenda Real Madrid na Barcelona.

Hii inamanaisha kwa sasa Liverpool itakuwa imekamilika katika maeneo yote uwanjani kuanzia golikipa na mashabiki wamekuwa wakiipa nafasi kubwa ya kuchuana na City katika mbio za ubingwa wa msimu ujao.

Manchester United imepewa nafasi ya tatu katika harakati za kuchukua ubingwa msimu ujao licha ya kushika nafasi ya pili katika msimu uliopita. Mpaka sasa imefanya usajili mkubwa mmoja tu kwa kumchukua kiungo wa mataifa wa Brazil, Fred, akitokea Shakhtar Donetsk kwa dau la Pauni 35 milioni.

Mwingine ambaye amechukuliwa na United katika dirisha hili ni pamoja na kinda wa Ureno, Diogo Dalot aliyenunuliwa kutoka Porto ya Ureno kwa dau la Pauni 18 milioni na ingawa amekuwa akitabiriwa kufanya makubwa katika jezi ya United, lakini anahitaji muda kuweza kuizoea ligi hiyo.

Chelsea imepewa nafasi mbele ya Tottenham na Arsenal baada ya kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi, lakini upepo unaweza kubadilika kutokana na kutoeleweka kwa hatima ya mastaa wake watatu, Eden Hazard, Thibaut Courtois na Willian ambao wanatajwa kutaka kuondoka Stamford Bridge.

Mpaka sasa imefanikiwa kumnasa staa wa kimataifa wa Italia mzaliwa wa Brazil, Jorginho, huku ikiwa inatazamiwa zaidi kuwa bize na dirisha hili kuanzia wiki hii baada ya hatima ya kocha kujulikana wiki iliyopita.

Wakati Tottenham ikiwa bado haijasajili mtu, upande wa Arsenal kumekuwa na ongezeko kubwa la matumaini baada ya kutua kocha mpambanaji, Unai Emery ambaye amenunua mastaa wanne huku akionekana kuwa na mbinu mpya kwa mujibu wa watu wa karibu na timu hiyo pamoja na video zinazoonekana mitandaoni.

Licha ya hayo ni Liverpool ndio ambayo iliyotumia pesa nyingi katika dirisha hili la uhamisho ikijaribu kutatua matatizo yake kwa kununua wachezaji mastaa.

Na ni suala la muda tu kuona kama kweli mastaa hao wataweza kutimiza matarajio ya mashabiki baada ya timu hiyo kutamba katika soko hili la uhamisho.