KUMBE WEPEESI: Liverpool yaipiga nyingi Man City, Arsenal ndo hivyo

Muktasari:

  • Mabao ya Alex Oxlade-Chamberlain, Roberto Firmino, Sadio Mane na Mohamed Salah yalitosha kudondosha mbuyu, Man City

LIVERPOOL,  ENGLAND

MUOSHA huoshwa. Si unakumbuka Manchester City iliipiga Tano Bila Liverpool kwenye ile mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England iliyofanyika Etihad?

Basi buana, Jurgen Klopp akanoa panga lake kumsumbiri Pep Guardiola huko Anfield na kilichotokea, Liverpool ikafanya kitu cha kutisha, ikapiga Man City 4-3.

Mabao ya Alex Oxlade-Chamberlain, Roberto Firmino, Sadio Mane na Mohamed Salah yalitosha kudondosha mbuyu, Man City ambayo ilikuwa haijapoteza mchezo wowote wa ligi hiyo tangu ilipoanza msimu huu na hivyo kumuonjesha Kocha Pep Guardiola kwa mara ya kwanza machungu ya kuchapwa.

Achana na hiyo kwanza. Tuhamie huko Emirates - Arsenal bila ya Alexis Sanchez na Mesut Ozil haiwezekani. Ndicho unachoweza kusema baada ya Kocha Arsene Wenger kuwapiga chini mastaa wake hao kwenye mchezo wa jana dhidi ya Bournemouth na kilichowakuta huko ni aibu.

Arsenal ikatangulia kufunga kwa bao la Hector Bellerin dakika ya saba tu baada ya kutoka mapumziko, lakini vijana wa Eddie Howe walicharuka na iliwaacha Gunners wafurahie uongozi wao kwa dakika 18 tu, kabla ya kuchomoa kwenye dakika 70 kupitia kwa staa wao Callum Wilson na dakika nne baadaye wakapiga bao la pili kupitia kwa Jordan Ibe, Arsenal inakufa 2-1. Kipigo hicho kinaifanya Arsenal iendelee kupaki basi lake kwenye nafasi ya sita ya msimamo wa ligi hiyo baada ya kukusanya pointi 39 katika mechi 23. Hicho ni kipigo cha sita kwa Arsenal kwa msimu huu na hivyo kuzidi kuweka rehani matumaini yao ya kumaliza ligi hii katika nafasi za juu,ikiwa imeachwa pointi kibao katika kuikamatia Top Four.

Kocha, Wenger aliamua kuwaweka kando kabisa ya kikosi chake mastaa wake wawili, Ozil na Sanchez, ambapo ripoti zinadai kwamba fowadi huyo wa kimataifa wa Chile yupo kwenye vita ya kuwaniwa na klabu za Manchester na huenda akachagua kujiunga na timu moja kati ya Manchester City au Manchester United. Liverpool nayo imeibuka kwenye vita ya kumtaka mshambuliaji huyo wa zamni wa Barcelona.

Haya twenzetu tena Anfield. Kwenye mechi hiyo Liverpool ilikuwa na hasira ya kulipa kisasi kutokana na udhalilishaji iliofanyiwa kwenye mechi ya kwanza, ilipopigwa 5-0 na hakika ililipa kisasi kwa kuwashushia vinara hao wa Ligi Kuu England kipigo kizito.

Unajua kilichotokea? Ni aibu. Bao nne zimetinga kwenye wavu wa Man City, huku mabao yote yakifungwa kwa uhodari mkubwa. Man City ilifunga mabao lake la kwanza kupitia kwa Leroy Sane. Liverpool ilikuwa wa kwanza kufunga kupitia kwa Chamberlain, lakini Man City ikachomoa kupitia kwa Sane na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Liverpool ilifunga mabao ya chapchap mara tatu kuiduwaza Man City, ambayo ilikuja kufunga mabao mengine ya haraka kupitia kwa Bernardo Silva, aliyeingia kutoka benchi na Ilkay Gundogan. Haikuwa mechi nzuri kwa Raheem Sterling, ambaye alikuwa akizomewa na Kop kila alipogusa mpira. Matokeo hayo bado yanaifanya Man City kuongoza ligi, lakini kama Manchester United itashinda mchezo wake wa leo Jumatatu dhidi ya Stoke City itapunguza pengo la pointi na kufikia 12 kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.