Liverpool wanapiga

Muktasari:

  • Liverpool imekuwa kwenye moto kweli kweli, kama ingekuwa gari basi lipo kwenye kasi kubwa na breki zimekata, ukikatiza mbele, basi utagongwa. Kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, Liverpool imecheza mechi tano na kushusha vipigo kwenye mechi zote hizo, ikiwamo ile ya jana Jumamosi, walipoifuata kwao Tottenham Hotspur na kuwachapa 2-1 uwanjani Wembley.

MWAKA wa Liverpool huu, ndicho unachoweza kusema kwa kile inachokifanya kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Liverpool imekuwa kwenye moto kweli kweli, kama ingekuwa gari basi lipo kwenye kasi kubwa na breki zimekata, ukikatiza mbele, basi utagongwa. Kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, Liverpool imecheza mechi tano na kushusha vipigo kwenye mechi zote hizo, ikiwamo ile ya jana Jumamosi, walipoifuata kwao Tottenham Hotspur na kuwachapa 2-1 uwanjani Wembley.

Mabao ya Georginio Wijnaldum na Roberto Firmino yalitosha kuihakikishia Liverpool mwanzo mzuri wa ligi kwa asilimia 100, huku kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kikifikisha pointi 15 na mabao 11. Bao la kujifariji la Spurs lilifungwa kwenye dakika za majeruhi na Muargentina, Erik Lamela.

Lakini, kipigo hicho kwa Spurs lawama zote zinaelekezwa kwa kipa Michel Vorm, ambaye alikuwa golini, akihusika kwenye mabao yote kutokana na kushindwa kuwa makini, huku akiifanya timu yake kupoteza mechi ya pili mfululizo.

Safu ya Spurs ilionekana kufanya makosa mengi sana na wangeweza kufungwa idadi kubwa zaidi ya mabao kama si lile bao la Firmino kukataliwa kwenye kipindi cha kwanza kwa madai kwamba Sadio Mane aliokuwa ameotea.

Mabeki hao wa kocha Mauricio Pochettino waliendelea kufanya makosa ambayo mwisho wa mechi yalikuja kuwagharimu, wakichapwa na kupoteza mwendo wao mzuri kwenye mchakamchaka wa ligi hiyo, ambapo walianza kwa kushinda mechi tatu za mwanzo, ikiwamo kuwachapa Manchester United 3-0 uwanjani Old Trafford.

Lakini, hii ni mara ya kwanza tangu msimu wa 1990-91 kwa Liverpool kushinda mechi tano za mwanzo wa msimu na hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili kwa Spurs kupoteza mechi mbili mfululizo katika Ligi Kuu England.

Kikosi cha Liverpool kilichoanza kwenye mechi hiyo na kuweka rekodi ya kushinda tu kiliundwa na Alisson, Alexander-Arnold, Gomez, Van Dijk, Robertson, Wijnaldum, Milner, Keita, Mane, Salah na Firmino.