Kuzuia wasihame ni kasheshe aisee

Muktasari:

Man United imechimba mkwara haiwezi kumwachia kipa huyo aondoke Old Trafford kama haitakuwa imempata Jan Oblak kutoka Atletico Madrid.

LONDON, ENGLAND. MAMBO ni kama hayazuiliki tena. Dele Alli anagoma kuifuta Manchester United kwenye mipango yake, huku David De Gea akijiandaa na safari ya Real Madrid.

Man United imechimba mkwara haiwezi kumwachia kipa huyo aondoke Old Trafford kama haitakuwa imempata Jan Oblak kutoka Atletico Madrid.

Sambamba na hilo, Kocha Jose Mourinho anakaribia kunasa staa mwingine kutoka Ureno baada ya Benfica kukubali ofa ya Pauni 35 milioni kumuuza staa wake Anderson Talisca.

Mambo ni moto kwenye dirisha hili la uhamisho na Liverpool nayo ilikuwa kwenye hatua za mwisho kumnasa staa wa Ufaransa, Nabil Fekir, huku presha ikiwa kubwa kuhusu Cristiano Ronaldo kuwa anaweza kufunguliwa mlango wa kutoka Real Madrid ili kunaswa Neymar wa PSG.

Mchakamchaka wa usajili ndani ya dirisha hili, unaweza kumhusisha pia Mohamed Salah, ambaye anaweza kupokea ofa ya usajili wa kushtukiza kutoka Barcelona, wakati Eden Hazard na Willian wakisubiri kufahamu hatima ya kocha kwenye kikosi chao cha Chelsea kabla ya kuchukua uamuzi wa kuihama timu hiyo ya Stamford Bridge huku majina yao yakitajwa huko Bernabeu na Old Trafford.

Kuna biashara pia inaweza kufanywa kuhusu mchezaji Anthony Martial kwenda Tottenham Hotspur, huku Mourinho akitaka huduma ya beki wa kati Toby Alderweireld licha ya mazungumzo ya kumnasa staa huyo kuwa kimya siku za karibuni.

Kiungo Mkenya, Victor Wanyama anaweza kujikuta sokoni kwa sasa huku Arsenal ikionekana bayana kuhitaji huduma ya kiungo huyo wa kati, licha ya kwamba saini yake inaweza kuziingiza timu nyingi vitani ikiwamo Chelsea.

Kasi hii ya uhamisho wa wachezaji hauzuiliki kwa sababu kila timu inatafuta namna ya kujitengeneza kwa ajili ya michuano ya ligi za msimu ujao ambapo Robert Lewandowski anaweza asiendelee kuwapo Bayern Munich huku ikidaiwa chochote kinaweza kutokea kuhusu Paul Pogba baada ya PGS na Juventus kuonyesha dhamira ya kuhitaji huduma ya kiungo huyo raia ya Ufaransa. Dirisha hili la usajili linaweza lisimwaache salama pia Antoine Griezmann huko Atletico na Ousmane Dembele kwenye kikosi cha Barcelona, wakali hao wanasakwa kwenye Ligi Kuu England na Nou Camp. Griezmann akitua Nou Camp, basi Dembele hawezi kubaki.

“Kwenye soka siwezi kusema hapana. Kama unavyojua mchezo huu chochote kinaweza kutokea,” alisema Dele Alli alipoulizwa kama anaweza kuihama Spurs mwaka huu huku Man United na Real Madrid zikitajwa mara kadhaa kwenye mpango wa kutaka huduma yake.