Kuna mafundi hawa, Lemar wanini Anfield!

Saturday February 10 2018

 

LIVERPOOL, ENGLAND. LIVERPOOL inaonekana kufunga mjadala kuhusu orodha ya mastaa inaowataka kuwasajili mwishoni mwa msimu na staa wa AS Monaco, Thomas Lemar jina lake limetupwa mbali kabisa.

Wababe hao wa Anfield wanatafuta mchezaji wa kuja kuchukua buti za Philippe Coutinho baada ya kumuuza mwezi uliopita kwenda Barcelona kwa ada ya Pauni 142 milioni.

Mwanzoni kulikuwa na ripoti inayodai Liverpool ilikuwa ikimtazama staa huyo wa Monaco kuwa mtu mwafaka wa kuchukua nafasi ya Coutinho, ambaye usiku wa juzi Alhamisi alifunga bao lake la kwanza huko Barcelona, wakati walipoichapa Valencia 2-0 kwenye Copa del Rey.

Baada ya wamiliki wa Liverpool kumpa Kocha Jurgen Klopp mzigo wa Pauni 75 milioni kuinasa saini ya Virgil Van Dijk, pesa nyingine nyingi inatarajiwa kutumika kwenye manunuzi ya mchezaji namba 10 au winga wakati dirisha kubwa la uhamisho wa wachezaji litakapofunguliwa mwisho wa msimu.

Baada ya kuweka kando mpango wa kumchukua Lemar, makala haya yanahusu mastaa wengine wanaofaa kabisa kunaswa na Liverpool kwenda kumaliza pengo lililoachwa na Coutinho kwenye klabu hiyo yenye maskani yake huko Anfield.

1. Christian Pulisic, B.Dortmund

Hakuna ubishi, Pulisic ni mmoja kati ya wachezaji wenye vipaji matata kabisa kuwahi kutokea kwenye mchezo wa soka kwa zama hizi za kisasa.

Kwa muda mrefu, Liverpool imekuwa ikimfukuzia staa huyo ambaye hakika amekuwa na kipaji na ufundi mkubwa anapokuwa na mpira ndani ya uwanja. Kitu kizuri kuhusu Pulisic ni umri wake ndiyo kwanza ana miaka 19, hivyo Liverpool itakuwa na muda wa kutosha tu kumtumia staa huyo kwa muda mrefu zaidi. Pulisic anaweza kucheza pande zote, kushoto na kulia, lakini pia anaweza kucheza katikati, kwenye namba 10 nyuma ya mshambuliaji wa kati.

2. Isco, Real Madrid

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amedai atampiga bei Isco kama ataendelea kubaki kwenye timu hiyo hadi msimu ujao. Jambo hilo linamfanya staa hiyo wa Kihispaniola kutokuwa na uhakika wa maisha yake huko Bernabeu, licha ya mwishoni mwa msimu uliopita kuwa kwenye sehemu muhimu kabisa ya kikosi cha Madrid ambapo panga pangua alikuwa hakosi namba kiasi cha kumfanya hadi James Rodriguez aondoke hapo kwenda Bayern Munich kwa mkopo wa miaka miwili.

Kwa hali ya Isco inayomkabili kwa sasa, Liverpool inaweza kufanya kweli na kwenda kuchukua huduma ambayo hakika itakuwa na msaada mkubwa kwelikweli kama itafanikiwa kuipata.

3. Malcom, Bordeaux

Winga huyo wa Kibrazili amekuwa akihusishwa na timu za Arsenal na Tottenham Hotspur katika dirisha la usajili lililofanyika mwezi uliopita.

Lakini, baada ya kushindwa kunaswa na timu yoyote hapo kati ya hizo, Liverpool inaweza kucheki uwezekano wa kuinasa huduma yake itakapofika mwishoni mwa msimu.

Shida ya Malcom ni kwamba anacheza eneo ambalo kwa sasa linachezwa na supastaa wa Anfield, Mohamed Salah, akitokea kulia na kutesa kwa mguu wake wa kushoto. Lakini, kwa staili ya kiuchezaji inayopendelewa na Klopp ya kutaka kushambulia na kumkaba mpinzani kwenye nusu yake, anaweza kumchukua Malcom na kisha kuwapanga na Mo Salah wote kwa pamoja, huku huduma yake ikiwa ya muda mrefu kwa sababu umri wa Malcom ndiyo kwanza miaka 20.

4. Oscar, Shanghai SIPG

Mtu aliyesahaulika kwenye soka la Ulaya baada ya kulipa kisogo mwaka mmoja uliopita alipokwenda kujiunga na Shanghai SIPG ya China kwa ada ya Pauni 60 milioni akitokea Chelsea.

Akiwa na umri wa miaka 26, kurejea kwenye soka ni kitu kinachosubiriwa kwa hamu kubwa kutokea katika kipindi cha usajili ujao kwa sababu ndiyo kwanza atakuwa kwenye wakati mwafaka wa kucheza soka la maisha yake.

Oscar si mchezaji wa kawaida hata Brazil wakati huo alikuwa akipata nafasi yeye mbele ya Coutinho, akichezeshwa Namba 10, eneo ambalo amekuwa akilimudu vizuri zaidi kuliko hata Mbrazili mwenzake huyo ambaye kwa sasa yupo Barcelona. Shida ya Oscar ipo kwenye mshahara wake, huko China analipwa Pauni 400,000, lakini kutakiwa na Liverpool kunaweza kumfanya akubali kushusha mshahara wake ili kurejea kwenye soka la Ulaya.

5. Nabil Fekir, Lyon

Amekuwa moto huko Olympique Lyon tangu Alexandre Lacazette alipoondoka kwenda Arsenal, sasa yeye ndiye amekuwa staa mkubwa kwenye kikosi hicho cha Wafaransa. Fekir ni mchezaji mwenye uwezo wa kuutawala mchezo anavyotaka na kupatata huduma yake kitakuwa kitu cha maana katika kikosi cha Liverpool huko Anfield.

Kwa msimu huu, Fekir amefunga mabao 16 na asisti tano kwenye Ligue 1 na kupata huduma yake hakika itaigharimu pesa nyingi kidogo Liverpool, kwa sababu anaonekana kuwa ndiye mchezaji kwenye thamani zaidi. Yeye na Isco katika orodha hii ndio wanaoweza kuifaa Liverpool katika kuziba pengo la Coutinho.