Kumbe shida Messi kwa Antonio Griezmann!

BARCELONA inapotajwa tu, basi jina la harakaharaka linalokuja akilini ni la Lionel Messi, labda hadi hapo Muargentina huyo atakapoondoka Nou Camp.

Neymar uvumilivu ulimshinda akaenda kuliweka jina lake kwenye chati za juu huko PSG na sasa imefichuka woga wa kwenda kufichwa na kivuli cha Messi ndilo suala linalodaiwa litazuia uhamisho wa Antonio Griezmann kwenda Barcelona.

Taarifa za kutoka Hispania zinadai Griezmann anahofu ya kwenda kuwa nyuma ya kivuli cha Messi atakapotua Barcelona na ndiyo maana hivi karibuni aliwaambia wachezaji wa Atletico Madrid haendi kokote.

Hata hivyo, mashabiki wa Atletico Madrid wanamwona kuwa ni kigeugeu na kuamua kumzomea katika mechi ya mwisho ya La Liga dhidi ya Eibar.

Mfaransa Robert Pires, alimwambia kama anataka kujitia kivuli kizito, basi aende tu Barca : “Kama anataka matatizo, changamoto ambayo asingependa kuikabili kwenye maisha yake, basi aende Barcelona. Ile ni timu nyingine kabisa.”