Kumbe ishu inaanzia kwa Hazard bana!

KINACHOELEZWA ni kwamba staa, Eden Hazard, ndiye anayetoa mchongo wa Antonio Conte afutwe kazi huko kwenye klabu ya Chelsea na badala yake achukuliwe kocha Maurizio Sarri.

Katika siku za karibuni, Hazard, ameonekana kutokuwa na furaha Chelsea na kuripotiwa kuwapiga mikwara mabosi wake akiwaambia kwamba kama hakutakiwa na mabadiliko yakiwamo kwenye kuongeza wachezaji wenye uwezo wa kupigania mataji, basi yeye atafikiria kuondoka.

Ripoti za karibuni zimedai Hazard ndiye anayechochea Chelsea wamchukue Sarri baada ya kuzungumza na Mbelgiji mwenzake, Dries Mertens, juu ya ubora wa kocha huyo ambaye ameondolewa kwenye kikosi cha Napoli hivi karibuni.

Conte bado anashikilia kibarua chake cha kuinoa Chelsea, lakini kwa ripoti zilizopatikana hadi kufikia jana ni kwamba The Blues walikuwa kwenye mazungumzo na Sarri na wanakaribia kufikia makubaliano.

Chelsea msimu huu imeshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na hivyo kukosa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini wakifanya msimu wao kumalizika vizuri kwa kubeba ubingwa wa Kombe la FA kwa kuwachapa Manchester United 1-0, shukrani kwa penalti ya Hazard kwenye fainali iliyofanyika Wembley wiki iliyopita. Taarifa za kutoka Italia zinadai Hazard amezungumza na Mertens kummegea makali ya Sarri na kilichozungumzwa hapo kimemvutia na kuonekana kuwashinikiza mabosi wa Chelsea wamchukue kocha huyo kwa sababu anafundisha mpira ambao yeye anapenda kuucheza. Habari zaidi zinadai Sarri ameshafahamu hata usajili wake atakaofanya baada ya kutua Chelsea.