King Pep

Tuesday May 15 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND

KATIKA suala la mchezaji mmoja mmoja, umekuwa msimu mzuri kwa staa wa Liverpool, Mohamed Salah. Lakini kwa suala la timu, ulikuwa ni msimu wa kushangaza kwa Manchester City chini ya kocha wake, Pep Guardiola. Klabu hiyo imezisambaratisha rekodi nyingi za Ligi Kuu England ambazo zilikuwa zimewekwa miaka ya nyuma.

ushinda mfululizo (18)

Kuanzia bao la ushindi la dakika za mwishoni la Raheem Sterling dhidi ya Bournemouth Agosti 26, mwaka jana mpaka suluhu ya bila kufungana dhidi ya Crystal Palace siku ya Mwaka Mpya, Manchester City ilikuwa imeweka rekodi ya kushinda mechi nyingi mfululizo katika Ligi Kuu England. Ilikuwa imeshinda mechi 18 mfululizo na kuisambaratisha rekodi ya Chelsea msimu wa 2016/17 iliposhinda mechi 13 mfululizo. Arsenal pia ilikuwa imeweka rekodi ya kushinda mechi nyingi mfululizo katika misimu miwili tofauti ya 2001/02 na 2002/2003 ambapo ilishinda mechi 14 mfululizo.

Pasi nyingi (902)

Hapa Manchester City ilivunja rekodi yake yenyewe. Katika mechi dhidi ya Chelsea Machi mwaka huu, iliweka rekodi ya kupiga pasi nyingi ndani ya mechi moja. Ilipiga pasi 902 na kuvunja rekodi yake ya awali iliyokuwa imeiweka katika pambano dhidi ya West Brom Oktoba, mwaka jana ambapo ilipiga pasi 843. Katika pambano hili la Chelsea, kiungo Ilkay Gundogan peke yake alipiga pasi 167 na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyepiga pasi nyingi ndani ya mechi moja katika historia ya Ligi Kuu England.

Mabao mengi katika msimu mmoja (106)

Hakuna timu iliyowahi kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja kama ilivyofanya Manchester City msimu huu. Baada ya bao la Gabriel Jesus katika pambano dhidi ya Southampton juzi, City imemaliza ligi ikiwa na mabao 106 ya msimu.

Imevunja rekodi iliyowekwa na Chelsea chini ya kocha, Carlo Ancelotti, msimu wa 2009/10 ambapo ilifunga mabao 103. Kifupi kwa msimu huu City ilikuwa na wastani wa mabao 2.3 kwa kila mechi.

Kushinda mechi (32)

Msimu uliopita ulikuwa wa Chelsea na tulishuhudia kocha mwingine Mtaliano wa Chelsea, Antonio Conte, akiweka rekodi ya kushinda mechi nyingi. Conte alishinda mechi 30 katika mechi 38 za ligi. Hata hivyo, Guardiola na vijana wake wamefanikiwa kuipiku rekodi hiyo na kushinda mechi 32 kati 38. Inakuwa timu ya kwanza kushinda mechi nyingi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England.

Pointi 100

Bao la dakika za mwishoni kabisa la Gabriel Jesus dhidi ya Southampton juzi, lilifungua ukurasa mpya katika historia ya Ligi Kuu England.

Liliifanya Manchester City kuwa timu ya kwanza kufikisha pointi 100 katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England. Awali, rekodi hiyo ilikuwa inashikwa na kikosi cha Chelsea chini ya kocha, Jose Mourinho. Katika msimu wa 2004/05, Chelsea ilifikisha pointi 95 na kusambaratisha utawala wa Manchester United na Arsenal katika enzi za Sir Ferguson na Arsene Wenger.

Kushinda ugenini (16)

Ushindi dhidi ya Southampton ulikuwa wa 16 katika mechi zao 19 za ugenini msimu huu. Hii ni idadi kubwa zaidi ya timu ya Ligi Kuu kushinda ugenini. Njiani, City ilipoteza ugenini katika mechi tatu tu dhidi ya Crystal Palace, Liverpool na Burnley. City walishinda mechi ngumu za ugenini dhidi ya Arsenal, Chelsea, United na Spurs.

Kwa kufanya hivyo ilikuwa imeipiku kwa mara nyingine rekodi iliyowekwa na Jose Mourinho na Chelsea yake katika msimu wa 2004/05 ambapo ilishinda mechi 15 ugenini.

Pointi ugenini (50)

Lazima umuheshimu Jose Mourinho kwa rekodi nyingi alizoweka katika msimu wa 2004/05. Alikuwa ameweka rekodi ya kukusanya pointi nyingi ugenini ambapo alikusanya pointi 48 katika msimu huo. Hata hivyo, msimu huu Manchester City imekusanya pointi 50 katika viwanja vya ugenini, ikiwa ni kubwa zaidi ya pointi za ugenini kwa msimu mmoja wa England.

Tofauti ya mabao (79)

Manchester City ilikuwa wakali katika kuziona nyavu, lakini ikawa nzuri pia kujilinda baada ya kutua kwa kipa Mbrazil, Ederson, kutoka Benfica. Msimu huu tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kwa Manchester City ni 79. Rekodi ya awali ilikuwa imewekwa na Chelsea msimu wa 2009/10 wakati ilipokuwa na tofauti ya mabao 71. Shukrani kwa mabao 29 yaliyofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier Drogba, ambaye msimu huo aliweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kuwa Mfungaji Bora Ligi Kuu England.

Mechi 5 mkononi (5)

Katika mechi tano za mwisho za msimu, wachezaji wa Manchester City walikuwa wakipigiwa makofi na wachezaji wa timu pinzani. Hii ni kwa sababu ya kuchukua ubingwa wakiwa na mechi tano na hivyo kuifikia rekodi ya watani wao Man. United ambao katika msimu wa 2000/01 walichukua ubingwa Old Trafford kwa kuichapa Coventry City mabao 4-2 huku wakiwa wamebakiza mechi tano. Nusura City msimu huu iipiku rekodi hii.