Mwamuzi agawa kadi kama njungu Brazil

Muktasari:

Matukio ya vurugu viwanjani imekuwa ni jambo la kawaida katika soka la Brazil

Bahia, Brazil. Soka la Brazil halijawahi kuishiwa vituko, kwa mara ya kwanza dunia imeshudia mwamuzi akitoa kadi nyekundu 10 na njano saba na kusababisha mchezo kuvunjika kati ya Vitoria dhidi ya Bahia katika ligi yajimbo la Bahia.

Baada ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilichojaa mshike mshike wenyeji Vitoria walipata bao la kuongoza kupitia Denilson, lakini mambo yalibadilika na kuwa mabaya zaidi baada ya vikosi vya timu mbili kurejea uwanjani kutoka mapumzikoni.

Bahia walipewa penalti katika dakika ya 50, jambo lililozua vurugu likaanza wakati wageni walipolipuka kwa shangwe na dansi mbele ya mashabiki wenyeji.

Wachezaji wa pande mbili wakakusanyika pamoja na kuanza kupigana makonde na baada ya mchezo huo kucheleweshwa kwa dakika 16, maafisa wakijaribu kutuliza hasira - mpiga kipenga akawafukuza uwanjani wachezaji wanane.

Kadi tatu zilitolewa kwa wachezaji wa Victoria na tano wakapewa wachezaji wa Bahia huku wachezaji wa akiba watatu wakiwemo miongoni mwa waliotolewa nje ya uwanja.

Mechi iliendelea, lakini baadaye mwamuzi alipowapatia wachezaji wawili wa Vitoria kadi nyekundu timu hiyo iliamua kuondoka uwanjani huku Bahia wakiwa na uwezekano wa kupewa ushindi wa 3-0.