Kachemka Mourinho alivyopukutisha mastaa wa maana Chelsea

Saturday February 10 2018

 

LONDON, ENGLAND. CHELSEA inapambana na hali yake kwa sasa huku kocha, Antonio Conte, akilalamika bodi imekuwa haifanyi usajili wa wachezaji anaowataka.

Wakati hilo likiendelea pale Stamford Bridge, kwa wapinzani wao Liverpool na Manchester City kuna mastaa, Mohamed Salah na Kevin De Bruyne, ambao wapo vizuri kweli kweli, lakini kumbe nyota hao walikuwa Chelsea, wakaondoshwa na Jose Mourinho.

Mourinho katika zama zake mbili alizofundisha Chelsea, aliwaondoa mastaa kibao aliowaona hawana maana, akiwamo Juan Mata. Cha ajabu sasa huko walikoenda mastaa hao wamefanya kweli na sasa mashabiki wa Chelsea wamebaki na majuto tu na kuishia kuwatamani, huku wengine klabu hiyo ikirudi kuwasajili tena.

Robert Huth

Beki huyo wa kati Mjerumani alionekana si kitu wakati alipokuwa Chelsea enzi za Mourinho. Akapigwa bei kwenda Middlesbrough kwa Pauni 6 milioni, hiyo ilikuwa Agosti 2006. Taratibu tu, Huth, alipandisha kiwango chake na kuwa bora kabisa akienda kuisaidia Leicester City kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2015.

William Gallas

Mourinho alimwona William Gallas si kitu na kuamua kumpeleka Arsenal katika dili la kubadilishana na Ashley Cole, ilikuwa Agosti 2006. Gallas alikwenda kucheza Arsenal kwa misimu minne na kisha kwenda Tottenham kwa miaka mitatu, huku kiwango chake kikimfanya aendelee kuitwa kwenye timu ya taifa ya Ufaransa aliyoichezea mechi 84. Gallas alikuwa msaada mkubwa huko kwenye timu nyingine alizokwenda.

Arjen Robben

Ni staa mwingine wa maana aliyeondoshwa Stamford Bridge na kuuzwa Real Madrid kwa ada ya Pauni 24 milioni Agosti 2007. Robben alidumu kwenye kikosi cha Chelsea kwa miaka mitatu na kucheza mechi 105, lakini akaonekana si kitu na kufunguliwa mlango wa kutokea.

Mdachi huyo aliondoka Madrid na kwenda kujiunga Bayern Munich, ambako amecheza soka la kiwango bora kabisa na kuipa timu hiyo mataji karibu kila msimu.

Glen Johnson

Glen Johnson aliichezea Chelsea, akapigwa bei kwenda Portsmouth kwa Pauni 4 milioni Agosti 2007. Miaka miwili baadaye klabu hiyo ikabaini imefanya makosa na kutaka kumsajili tena, lakini beki huyo wa kulia aliamua kutimkia Liverpool, alikojiunga kwa ada ya Pauni 18 milioni baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa huko Pompy.

Akaenda Stoke City na alikuwa panga pangua akicheza beki wa kulia wa England katika fainali za Kombe la Dunia 2010 na 2014.

Kevin De Bruyne

De Bruyne yupo kwenye ubora wake huko Etihad. Lakini, kabla ya hapo aliwahi kuwa Chelsea, alikoonekana si kitu na kupigwa bei Wolfsburg kwa Pauni 18 milioni, Januari 2014 baada ya Mourinho kushindwa kumpa nafasi, akicheza mara tatu tu kwenye Ligi Kuu England.

Alipokuwa Ujerumani, De Bruyne, alicheza soka la kiwango bora kabisa kiasi cha kuwafanya Manchester City kwenda kumsajili kwa Pauni 55 milioni Agosti 2015 na tangu hapo hadi sasa amekuwa moto uwanjani, hata Chelsea wenyewe wanamuogopa.

David Luiz

Beki, David Luiz, aliondolewa Chelsea na kocha Mourinho na kuuzwa PSG kwa Pauni 50 milioni Juni 2014. Mourinho hakujali kama Mbrazili huyo alikuwa kipenzi cha mashabiki. Baada ya miaka miwili, Chelsea walikwenda kumnunua tena Luiz kwa ada ya Pauni 34 milioni. Hiyo ilikuwa Agosti 2016 baada ya timu hiyo kuwa chini ya kocha, Antonio Conte na aliwasaidia kubeba taji la Ligi Kuu England.

Romelu Lukaku

Alinaswa na Chelsea akitokea Anderlecht 2011 wakati huo akiwa ndiyo kwanza ana miaka 18. Akacheza mechi tatu tu chini ya Mourinho kabla ya kutolewa kwa mkopo na baadaye kuuzwa kwenda Everton kwa ada ya Pauni 28 milioni Julai 2014.

Mwaka jana, Chelsea ilitaka kumsajili, lakini Mourinho akiwa huko Man City, aliamua kuiwahi huduma yake kwa Pauni 75 milioni, na ameshafunga mabao 19 katika mechi 36.

Mohamed Salah

Aliondoshwa na Mourinho huko Stamford Bridge akimuuza AS Roma kwa Pauni 12 milioni, Julai 2016 baada ya kumtoa kwa mkopo mara kadhaa Roma na Fiorentina. Mwaka jana alinunuliwa na Liverpool kwa Pauni 37 milioni na tangu wakati huo amekuwa moto uwanjani akifunga mabao 21 kwenye Ligi ya EPL.