KIBURI Liverpool yavunja rekodi ya uhamisho ya makipa

Muktasari:

Hatimaye Liverpool imefanikiwa kumnasa kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Brazil na AS Roma, Alisson kwa kiasi cha Pauni 67 milioni ambacho kinavunja rekodi ya uhamisho wa makipa duniani. Ni jeuri kubwa ya pesa.

MERSEYSIDE, ENGLAND. KWENYE udhia penyeza rupia. Mwezi Januari Liverpool ilitatua tatizo la beki kwa kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia ilipomnunua Virgil van Dijik. Safari hii imetatua tatizo la kipa kwa kuvunja rekodi ya uhamisho wa makipa.

Hatimaye Liverpool imefanikiwa kumnasa kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Brazil na AS Roma, Alisson kwa kiasi cha Pauni 67 milioni ambacho kinavunja rekodi ya uhamisho wa makipa duniani. Ni jeuri kubwa ya pesa.

Staa huyo wa Brazil amelazimika kukatisha likizo yake katika Visiwa vya Sardinia kwa ajili ya kwenda Liverpool juzi Jumanne na jana alitazamiwa kupimwa afya Anfield kabla ya kusaini mkataba wa miaka sita na wababe hao waliokuwa na tatizo la kipa.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Liverpool, Michael Edwards alifikia makubaliano na mkurugenzi mwenzake wa ufundi wa Roma, Monchi ambapo sasa Liverpool italipa kiasi cha Pauni 58.5 milioni mbele kisha kumalizia Pauni 9 milioni baadaye.

Awali ofa ya Pauni 62 milioni ya Liverpool ilikataliwa na Roma lakini Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp hakuona umuhimu wa kupoteza muda na kuanza kusumbuana na Chelsea na Real Madri ambazo pia zilikuwa zinamtaka kipa huyo. Ikamalizia ilichotaka Roma.

Uhamisho wa Alisson kwa sasa unakuwa mara mbili ya rekodi ya awali ya uhamisho wa makipa ambayo iliwekwa na kipa wa Manchester City, Ederson aliyehamia klabuni hapo kwa dau la Pauni 35 milioni miezi 12 iliyopita. Ederson ni kipa wa pili katika kikosi cha Brazil.

Hakutarajiwi kuwa na matatizo yoyote katika mazungumzo ya maslahi binafsi baina ya kipa huyo na Liverpool na klabu hiyo imedhamiria kumtangaza Alisson kama usajili wake wa nne katika dirisha hili kabla haijaondoka kwenda Marekani leo Ijumaa kwa maandalizi ya msimu mpya.

Hata hivyo, kipa huyo hataungana na wenzake katika ziara hiyo ambayo itaiona Liverpool ikicheza dhidi ya Manchester United, Manchester City na Borussia Dortmund kwa vile ana wiki nzima ya kuendelea na likizo yake baada ya Brazil kufika robo fainali katika Kombe la Dunia.

Kuwasili kwa kipa huyo kunamaanisha huenda ukawa mwisho wa kipa, Loris Karius ambaye alikuwa anaaminiwa na Kocha Klopp lakini akafanya makosa katika pambano la fainali za Ulaya dhidi ya Real Madrid Mei mwaka huu na hata katika mechi za maandalizi ya msimu mpya.

Klopp alikuwa anataka kumpa nafasi nyingine Karius lakini hakukuwa na dalili za kipa huyo kujirudi baada ya kurudia makosa katika pambano la kirafiki dhidi a Tranmere Jumanne usiku na hatimaye mabosi wa Liverpool waliamua kuvunja rekodi ya uhamisho kwa Alisson ambaye walikuwa wanamfukuzia tangu Januari.

Chelsea ilikuwa imeingia katika mbio za kumnasa Alisson baada ya kugundua kuwa kipa wake, Thibaut Courtois anaelekea Real Madrid lakini pia Alisson anafahamika kwa kocha mpya wa timu hiyo, Maurizio Sarri.

Inasemekana Alisson alishawishiwa kwa kiasi fulani na staa mwenzake wa Brazil, Roberto Firmino ambaye alikuwa naye katika kikosi cha Timu ya Taifa kule Russia.

Usajili wake unaweza kuwa wa mwisho kwa Liverpool katika dirisha hili baada ya kufanikiwa kuwanasa Naby Keita kutoka RB Leipzig, Xherdan Shaqiri kutoka Stoke na Fabinho kutoka Monaco. Dili la kumnasa Nabil Fekir kutoka Lyon lilikwama.

Kulikuwa na uvumi huenda dili la Fekir likarudi lakini kama likirudi basi Liverpool italazimika kupunguza kikosi chake kwa sasa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wachezaji.