Juventus yamtaka beki wa Arsenal

Saturday November 11 2017

 

London, England. Juventus imerusha ndoano kutaka saini ya mchezaji wa Arsenal, Hector Bellerin.
Taarifa za awali, zimedai kuwa beki huyo wa kulia anaweza kuondoka Arsenal katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.
Juventus ‘Kibibi Kizee cha Turin’ imekutana na wawakilishi wa beki huyo kuzungumzia usajili huo na huenda pande hizo zikafika mwafaka.
Mabingwa hao wa Italia, wamevutiwa na kiwango cha mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania kwenda kuziba pengo la Dani Alves aliyetimkia Paris Saint Germain (PSG).
Habari hizo zinaweza kuwa chungu kwa kocha Arsene Wenger anayekabiliwa na kibarua kigumu kubakiza nyota wawili Alexis Sanchez na Mesut Ozil.
Juventus imetamba kutoa fedha ya maana kupata saini ya beki huyo mwenye uwezo mzuri wa kukaba katika eneo la ulinzi.
Licha ya kumsajili beki Mattia De Sciglio kutoka AC Milan, Juventus haijapata mrithi sahihi wa nafasi hiyo tangu alipoondoka Alves.