Jinsi ya kutibu wachezaji majeruhi

Muktasari:

Pamoja na straika huyo aliyebeba tumaini la Wamisri na Waafrika pia wakati wa kuelekea fainali hizo kufunga kwa penati katika mchezo huo, lakini hakuweza kubadili matokeo kwani walilala mabao 3-1.

STRAIKA machachari wa Misri aliyetokea benchi la majeruhi, Mohmed Salah, Jumanne alijumuishwa katika kikosi kilichoanza mchezo wa pili wa timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia. Ilikuwa katika mechi ya Kundi A dhidi ya wenyeji Russia.

Pamoja na straika huyo aliyebeba tumaini la Wamisri na Waafrika pia wakati wa kuelekea fainali hizo kufunga kwa penati katika mchezo huo, lakini hakuweza kubadili matokeo kwani walilala mabao 3-1.

Achana na mambo hayo ya matokeo. Naamini unakumbuka mchezaji huyu aliumia bega kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya alipokuwa na klabu yake Liverpool dhidi ya Real Madrid mwishoni mwa mwezi uliopita. Jeraha hilo ndilo lililomkosesha mechi ya kwanza ya Misri dhidi ya Uruguayi wiki iliyopita.

Salah ni mmoja wa wachezaji waliojumuishwa katika timu zao za taifa za Kombe la Dunia kule Russia licha ya kuwa majeruhi, mastaa wengine ni pamoja na Harry Kane (England), Manuel Neuer (Ujerumani) na Kun Aguero (Argentina).

Katika mechi ya Brazili dhidi ya Iceland ya sare ya bao 1-1, Neymar aliingia katika rekodi baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kwa kipindi cha miaka 20 kufanyiwa faulo nyingi kuliko yeyote. Siku tatu baadaye, kiungo huyo wa PSG alionekana akichechemea wakati akitoka mazoezini. Alipoulizwa kulikoni, alijibu hajaumia sana bali ni maumivu madogo tu.

Kikosi cha England nacho kimepata pigo baada ya mshambuliaji wake Delle Alli kukumbwa na maumivu ya misuli ya paja wakati wa mechi dhidi ya Tunisia.Taarifa zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo anayeichezea Tottenham huenda akazikosa mechi zote zilizobakia kutokana na majeraha hayo.

Katika mchezo huo ambao Tunisia iliambulia kipigo cha mabao 2-0, timu hiyo pia ilimpoteza kipa namba moja, Mouez Hassen, aliyepata majeraha ya bega.

Alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Ben Mustapha, kipa ambaye muda mwingi huwa hapewi nafasi.

Ni kawaida majeraha ya kimichezo kuwapata wachezaji katika mashindano makubwa kama haya yenye upinzani mkali na ufundi wa kila namna, kwani hutumia nguvu nyingi kucheza au kukaba, hivyo kujikuta wakigongana kimwili, kuchezewa faulo au kujijeruhi wenyewe.

Timu zote zinazoshiriki Kombe la Dunia huwa na jopo la wataalamu wa afya wanaotoa huduma za ushauri na matibabu kwa wachezaji wanaopata majeraha.

Kijumla kuna mambo kadhaa yanayofanyika ili kuhakikisha majeruhi anapona kwa wakati, kama kupumzika, kushikamana na ushauri ule wa kimatibabu, kula mlo kamili, majaribio ya uchunguzi baada ya kupona, mazoezi mepesi ya viungo, mazoezi binafsi ya mchezo na hatimaye kujiunga na mazoezi ya timu.

Majeruhi hupewa mapumziko na huondolewa katika mazoezi ya timu na hutakiwa kutumia muda mwingi kupumzika. Hushauriwa kulala kwa kati ya saa sita hadi nane kwa siku ili kuupa mwili fursa ya kujikarabati hivyo kuepukana na mambo yanayoweza kutonesha jeraha au kujijeruhi upya.

Kama kuna dawa za matibabu au virutubisho lishe na maelekezo ya wataalamu wa afya, majeruhi hutakiwa kushikamana nayo kipindi chote cha uuguzi.

Ushauri wa wataalamu ndio msingi wa kupona majeraha kwa wakati na mhusika kurudi mchezoni akiwa imara kama hapo awali.

Kipindi cha uuguzi wa jeraha, mchezaji hupewa mlo kamili yaani mlo uliosheheni makundi yote ya vyakula na ulioandaliwa kwa kufuata kanuni za afya.

Hupangiwa ratiba maalumu ya lishe ikiwamo muda wa kula milo yake mikuu minne na milo midogo midogo. Hivi ni vile vyakula vya katikati ya milo mikuu, kitaalamu huitwa ‘snacks’. Mfano wa snacks ni pamoja na matunda, juisi na vyakula jamii ya karanga.

Kwa majeruhi wa michezo, hupewa vyakula vya protini kwa wingi hasa samaki na vile vya jamii ya kunde. Ni kwa sababu vyakula hivi vimejaa protini nyingi. Ikumbukwe kuwa protini ndio kirutubisho chenye kazi ya kujenga mwili, hivyo husaidia ukarabati wa jeraha na kuunga vizuri.

Hushauriwa kula mboga na matunda kwa wingi kwani vyakula hivi huwa na vitamini, madini na virutubisho muhimu kwa kujenga kinga imara ya mwili. Kinga ndiyo kila kitu mwilini. Kinga imara husaidia kukarabati jeraha kwa haraka na vile vile kulinda mwili dhidi ya uvamizi wa vimelea vya maradhi.

Hushauriwa kunywa maji mengi ili kuepukana na upungufu wa maji na kukosekana usawa wa chumvi chumvi za mwilini, uwepo wa mambo haya mawili huaathiri utendaji wa mwili kiujumla.

Upungufu wa maji mwilini huweza kusababisha tatizo la kukakamaa kwa misuli, hivyo kuongeza hatari ya kuongezeka kwa ukubwa wa jeraha.

Wataalamu lishe huwa karibu na wachezaji majeruhi kwa lengo la kufuatilia kwa karibu lishe yao na maendeleo yao ya kiafya.

Huwapa virutubisho lishe maalumu vya ziada vilivyotengenezwa kitaalamu, virutubisho hivi husaidia mwili kupata viambata muhimu vinavyohusika katika shughuli za mwili ikiwamo ukarabati wa jeraha.

Hupimwa uzito mara kwa mara ili kuona kama kuna ongezeko holela la uzito, uwepo wa uzito mkubwa huongeza hatari ya kujijeruhi, hii ni kutokana na shinikizo kubwa la uzito wa mwili. Tatizo la kuongezeka uzito hudhibitiwa kwa kushauriwa kula vyakula rafiki visivyonenepesha mwili.

Huwekwa katika mazingiria mazuri ambayo huwapa utulivu wa kimwili na kiakili ili wasipate matatizo yoyote ikiwamo shinikizo la kikakili au msongo wa mawazo.

Matatizo haya yakitokea husababisha kinga ya mwili kutetereka, hivyo jeraha huwa katika hatari ya kuchelewa kupona.

Kwa kawaida usafi wa mazingira wanayoishi majeruhi huwa ni wa hali ya juu huku wakishauriwa kuwa wasafi kimwili pia kuepukana na uvamizi wa maradhi mengine mwilini.

Husimamiwa kufuata mienendo na mitindo bora ya kimaisha kama vile kuepuka ulevi, uvutaji sigara au matumizi ya vilevi vingine. Vitu vya aina hiyo vikitumiwa na mchezaji majeruhi, huudhoofisha mwili wake hivyo jeraha huchelewa kupona.

Inashauriwa kutoa taarifa mapema pale mhusika anapoona mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida mwilini au katika jeraha. Baadaye anapochunguzwa kwa kina kama hana maumivu, hupewa majaribio mbalimbali kuthibitisha kupona kwake. Akibainika amepona, taratibu huanzishiwa programu binafsi ya mazoezi mepesi na mazoezi ya viungo.

Kipindi chote cha kuuguza jeraha, huduma za usingaji mwili (massage), kuogelea na mazoezi ya ‘gym’ hutolewa kwa mhusika, lengo ni kuisaidia misuli na viungo vya mwili kurudi katika uimara wake.

Mwisho akiwa fiti na kupona kabisa hurudishwa katika mazoezi ya pamoja ya timu.

Hayo ni baadhi ya mambo ya msingi ambayo wachezaji wa kimataifa hufanyiwa na hivyo kuwezeshwa kupona kwa wakati na kurudi uwanjani wakiwa katika viwango vyao vya awali.