Ian Wright: Ozil akitua Man Utd atakuwa amazing!

Friday January 12 2018

 

LONDON, ENGLAND

STAA wa zamani wa Arsenal, Ian Wright amesema kama kuna sehemu ambayo Mesut Ozil atakwenda kuwa mtamu na kila mtu atampenda kwa soka lake basi ni Man United. Ian Wright, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka alisema Ozil akienda Man United atakuwa kwenye kikosi kitakachompa uhuru wa kucheza kandanda lake safi kuliko hata anavyofanya Emirates kwa sasa. Kiungo huyo wa Kijerumani atapatikana bure kabisa mwishoni mwa msimu na ripoti zilizopo ni kwamba, atakwenda Old Trafford kuungana na kocha wake wake wa zamani Jose Mourinho, ambaye aliwahi kumnoa wakati walipokuwa Real Madrid.

Wakati Alexis Sanchez akipanga pia kuachana na Arsenal na kutimkia Manchester City, gwiji huyo wa The Gunners, Wright alikiri kuumizwa sana na hilo na kusema hasa huyu Ozil, akienda Man United, kwamba Arsenal watajuta kumfahamu.

Ian Wright aliulizwa kama anahisi Ozil atafiti Man United na kusema: “Ndiyo, haswa atafiti vizuri sana. Mchezaji wa aina ya Ozil atakufurahisha tu. Hasa kwa wachezaji wale atakaokwenda kucheza nao Man United, nawaambia atakuwa moto.”