Hiyo Arsenal ya Emery msimu ujao, mjipange

Muktasari:

Si unajua Kocha Emery anataka kuwafanya mashabiki wa Arsenal kusahau kile kipindi kigumu walichopitia mwishoni mwa miaka ya Kocha Arsene Wenger katika kikosi hicho chenye maskani yake Emirates.

LONDON, ENGLAND. ILE kipyenga pyee kwenye Ligi Kuu England, Kocha Unai Emery atashusha mziki huo, nakwambia Manchester City wanapaswa kujipanga kweli kweli, la itakuwa aibu.

Si unajua Kocha Emery anataka kuwafanya mashabiki wa Arsenal kusahau kile kipindi kigumu walichopitia mwishoni mwa miaka ya Kocha Arsene Wenger katika kikosi hicho chenye maskani yake Emirates.

Tangu alipotua Arsenal, Kocha Emery amekuwa akifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kwa kusajili wachezaji ambao anaamini wakitua watakuja kuifanya timu hiyo kuwa tofauti kabisa.

Emery ameshawanasa viungo wawili, Lucas Torreira, ambaye anakaba huyo kama N’Golo Kante, amemnasa pia Matteo Guendouzi, huku amenyakua pia mabeki wawili, Sokratis Papastathopoulos na Stephan Lichtsteiner, ambao wote ni wazoefu na kipa Bernd Leno.

Na bado hajafunga usajili, ambapo kwa sasa ameripotiwa kuwasaka mastaa kama Steven Nzonzi na Ever Banega kuhakikisha Arsenal inakuwa na kikosi matata kinachoanza na wale watakaokuwa kwenye benchi.

Kama mambo yatabaki kama yalivyo, hakuna mchezaji mwingine atakayesajili, basi Emery kwenye mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England, anaweza kuanza na fomesheni ya 4-3-2-1, ambapo golini atasimama Leno, huku mabeki wake wanne kushoto atakuwa Kolasinac, kushoto Bellerin na kati ni Chambers na Sokratis.

Hapo kwa sababu Laurent Koscielny bado majeruhi, akipona tu, basi Chambers itabidi asubiri kwenye benchi.

Kwenye kiungo kutakuwa na pini tatu matata, Xhaka atakayekuwa upande wa kushoto, Ramsey upande wa kulia na kati, mbele kidogo ya mabeki wa kati, atasimama Torreira kufanya kazi ya kukata umeme.

Kwenye fowadi, Ozil atakuwa upande wa kushoto na kulia ni Mkhitaryan huku Aubameyang akiwa mbele kabisa kufanya jambo moja tu, kuzitendea hadi pasi zitakazotoka kwa wakali hao kuhakikisha zinatinga kwenye nyavu za wapinzani.

Hapo Alexandre Lacazette na wakali wengine akiwamo Danny Welbeck watakuwa wanasubiri kwenye benchi. Mkakati wa Emery ni kuhakikisha Arsenal inarudi ndani ya Top Four kwa msimu ujao.