Hazard atengewa jezi namba 7 Madrid

Muktasari:

Jezi namba 7 imekuwa na heshima kubwa huko Real Madrid na ilikuwa ikivaliwa na Cristiano Ronaldo na kabla ya hapo ilikuwa kwenye mwili wa gwiji, Raul.

REAL Madrid wameripotiwa wanafanya kila wanaloweza kumshawishi Eden Hazard kung’oka Stamford Bridge na kwenda Bernabeu baada ya kuwambia wamemwandalia jezi namba 7 akienda kujiunga na Los Blancos.

Jezi namba 7 imekuwa na heshima kubwa huko Real Madrid na ilikuwa ikivaliwa na Cristiano Ronaldo na kabla ya hapo ilikuwa kwenye mwili wa gwiji, Raul.

Kwa Hazard kwenda moja kwa moja Real Madrid na kukabidhiwa jezi hiyo hilo litakuwa na heshima kubwa kwake na hapo atakuwa amepewa hadhi ya moja kwa moja ya kurithi mikoba ya Ronaldo, ambaye ametimkia kwenye kikosi cha Juventus.

Staa huyo wa Kibelgiji ameripotiwa kuwekwa mstari wa mbele kwenye ile orodha ya wachezaji wanaosakwa na Real Madrid ili kwenda kufanya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kuwa na makali kwa ajili ya msimu ujao.

Baada ya kutoka kwenye fainali za Kombe la Dunia, Hazard anaaminika kwamba atahama London kwenye dirisha hili la usajili huku Don Balon likiripoti Los Blancos sasa wamejipanga kwa kila kitu kwenda kumchukua mtu wao. Kwa sasa kilichobaki ni suala la Chelsea na Real Madrid kukubaliana tu kwenye ada ya uhamisho licha ya kuwapo na taarifa za kwamba ada ya Pauni 170 milioni ili kubalika na pande zote mbili.

Kwenye kikosi cha Chelsea, Hazard anavaa jezi namba 10, lakini huko Real Madrid jezi hiyo inashikiliwa na Luka Modric, ambaye kiwango chake cha kwenye Kombe la Dunia kimedaiwa kuifanya jezi hiyo kununuliwa kwa wingi na mashabiki wa Real Madrid huko dukani.