Fekir bado anaitaka Liverpool unaambiwa

Tuesday June 12 2018

 

UNAAMBIWA hivi, Nabil Fekir hataki kukubali kama dili la ndoto zake la kutua Liverpool limekufa, hivyo hataki kuifungia milango miamba hiyo ya Anfield na kufichua wakirudi tena mezani anatua tu bila ya kuweka ngumu yoyote.

Staa huyo wa Olympique Lyon, Fekir alikaribia kabisa kujiunga na Liverpool akiripotiwa hadi kupima afya kabla ya kila kitu kutibuka baada ya vipimo vya afya na kufanya usajili huo kusitishwa.

Shida kubwa iliyoelezwa ni Fekir, ambaye kwa sasa yupo na Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia aliwahi kuumia huko siku za nyuma kitu ambacho kilionekana kwenye vipimo alivyofanyiwa Liverpool na kufanya usajili huo kusitishwa.

Ripoti zinafichua kiungo huyo amehuzunishwa sana na dili hilo kutibuka, taarifa ambazo zimemfikia Kocha Jurgen Klopp, mchezaji huyo moyo wake bado unahitaji kutua Anfield.

Kama Liverpool wataamua kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Fekir atawafikiria wao kwanza kabla ya kufikiria kwenda kujiunga na timu nyingine. Staa huyo amekuwa akiwindwa pia na Bayern Munich na Atletico Madrid.