Eti Conte kuishtaki Chelsea

Muktasari:

Kocha huyo Mtaliano alifunguliwa mlango wa kutokea Stamford Bridge wiki iliyopita, ikiwa ni siku 55 zimepita tangu msimu wa 2017-18 ulipokwisha huku Chelsea ikifanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la FA.

KINACHOELEZWA ni, Kocha Antonio Conte ana mpango wa kuwapeleka mahakamani waajiri wake wa zamani Chelsea kuwashtaki kwa nini walitumia siku nyingi kumfukuza kazi.

Kocha huyo Mtaliano alifunguliwa mlango wa kutokea Stamford Bridge wiki iliyopita, ikiwa ni siku 55 zimepita tangu msimu wa 2017-18 ulipokwisha huku Chelsea ikifanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la FA.

Chelsea walikwama kwenye mpango wa kumchukua Maurizio Sarri, kocha waliyekuwa wakipiga hesabu za kuja kurithi mikoba ya Conte huko Chelsea kwa sababu alikuwa bado ni mwajiri wa Napoli.

Baada ya kuununua mkataba wa Sarri ndipo wababe hao wa Ligi Kuu England walipoweza kumpata kocha huo na hivyo kumpiga chini Conte licha ya kuwa na mwaka mmoja uliobaki kwenye mkataba wake.

Kutokana na hilo, Conte ameshaweka mfukoni Pauni 9 milioni za fidia ya mkataba wake kuvunjwa, lakini kilichomkera ni kitendo cha Chelsea kuchukua muda mrefu kumwachia wakati tayari walikuwa na mpango huo wa kumfuta kazi mapema tu.

Wasiwasi wa Conte ni, kwa muda ambao Chelsea wamemwaacha anaweza asipate kazi mpya hadi mwakani.