Eti Alexis apigwe tu chini United

Muktasari:

Scholes anachoamini, Mourinho anapaswa kuwaanzisha Marcus Rashford na Anthony Martial kwenye mechi hiyo kusaidiana na straika Romelu Lukaku.

GWIJI wa Manchester United, Paul Scholes amemwambia Jose Mourinho kama kuna mchezaji anayepaswa kupigwa chini katika kikosi chake kitakachocheza na Tottenham Hotspur kwenye nusu fainali ya Kombe la FA basi ni Alexis Sanchez.

Scholes anachoamini, Mourinho anapaswa kuwaanzisha Marcus Rashford na Anthony Martial kwenye mechi hiyo kusaidiana na straika Romelu Lukaku.

Mwingereza huyo anaamini kufanya hivyo Man United itakuwa na makali zaidi ndani ya uwanja kuliko kumwanzisha Sanchez, ambaye alinaswa na Kocha Mourinho katika dirisha la Januari akitokea Arsenal.

“Nadhani uamuzi mkubwa kabisa utakuwa nani wa kucheza kushoto na kulia kwa Romelu Lukaku,” alisema Scholes.

“Mimi ningewachagua (Marcus) Rashford na (Anthony) Martial, lakini ninachokiona yeye atamwanzisha Sanchez.

“Sidhani kama kiwango chake kipo vizuri. Nadhani kwa sasa Sanchez anatabirika. Man United ina wachezaji wenye vipaji sana, lakini haijataka tu kuwatumia waonyeshe uwezo wao.

“Kwa upande wangu nadhani Martial na Rashford wangekuwa chaguo zuri.”