Enrique: Messi? Ile ni shida

Muktasari:

Kauli ya Enrique imekuja baada ya Messi kuwekwa kando katika tuzo za Fifa za Mchezaji Bora wa Mwaka na kudhihirisha mchakato huo wa kugawa tuzo za ubora wa soka unafanywa kisiasa.

KOCHA wa Hispania, Luis Enrique amepata nafasi ya kumnoa Lionel Messi huko Barcelona na amekuwa na jambo moja tu kuwaambia wale ambao hawajahi kufanyakazi au kuwa karibu na supastaa huyo wa Argentina ni mchezaji aliyewaacha wenzake mbali sana kwa ubora.

Kauli ya Enrique imekuja baada ya Messi kuwekwa kando katika tuzo za Fifa za Mchezaji Bora wa Mwaka na kudhihirisha mchakato huo wa kugawa tuzo za ubora wa soka unafanywa kisiasa.

Wachezaji watatu walioingia fainali kuwania tuzo hiyo ni Cristiano Ronaldo wa Juventus, Mohamed Salah wa Liverpool na kiungo Luka Modric wa Real Madrid.

Tuzo hiyo itatolewa mwezi huu kwenye sherehe zitakazofanyika London, England.

Kocha huyo alisema hilo wakati kikosi chake kilipokuwa kikijiandaa na mechi ya UEFA Nations League, ambapo La Roja iliichapa Croatia 6-0 na Enrique alisema: “Kama nitawazungumzia Croatia, basi wachezaji wake ni Modric na Ivan Rakitic. Wawili hao wote wanahitaji kupewa tuzo. Lakini, kama nitamzungumzia mchezaji bora wa dunia, basi tuzo hiyo ya mchezaji bora inamhusu Leo Messi, kwa sababu yupo hatua moja mbele kuliko wengine.”