Emery alipotembelea uwanja wa mazoezi

Muktasari:

Siku chache tu baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa Arsenal, tayari kocha huyo ameshafanya ziara ya kutembelea uwanja wa mazoezi wa timu hiyo kuona mambo yalivyo, ikiwa ni siku yake ya kwanza tu kuanza kazi kwenye kikosi hicho, tangu alipotajwa kuwa kocha mpya klabuni hapo.

LONDON, ENGLAND. UNAI Emery kweli kazi anaitaka. Anaonekana kukipokea kibarua cha kuchukua mikoba ya Arsene Wenger kwa furaha kweli kweli.

Siku chache tu baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa Arsenal, tayari kocha huyo ameshafanya ziara ya kutembelea uwanja wa mazoezi wa timu hiyo kuona mambo yalivyo, ikiwa ni siku yake ya kwanza tu kuanza kazi kwenye kikosi hicho, tangu alipotajwa kuwa kocha mpya klabuni hapo.

Emery, aliyetoka kuinoa PSG, alikwenda kuonyeshwa vifaa vya kufanyia mazoezi vilivyopo uwanjani, Colney, juzi Alhamisi. Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Vifaa, Sean O’Connor, ndiye alimpitisha kocha huyo kwenye uwanja huo wa mazoezi kujionea mambo yalivyo.

Emery ndiye kocha wa Arsenal kwa sasa akichukua nafasi ya Wenger, ambaye alidumu kikosini humo kwa miaka 22 na kufanikiwa kuwapa mataji matatu ya Ligi Kuu England.

Mhispaniola huyo alionekana kuwa kwenye hali nzuri alipoonekana akiwa na kikombe chake cha kahawa. Katika ziara yake uwanjani hapo, Emery alikutana na beki wake wa kati, Laurent Koscielny, ambaye alikuwa kwenye chumba cha viungo akifanyishwa mazoezi ili kupona haraka majeraha yake ya enka.

Ukiweka kando chumba cha matibabu, Emery, alipitishwa pia kwenye gym, vyumba vya kubadilishia, viwanja vya ndani pamoja na ofisi tofauti.

Wakati anatambulishwa Jumatano iliyopita, Emery, aliahidi kuleta soka lenye mvuto na mataji yataanza kurudi tena Emirates.

“Bodi inajua malengo yangu na mipango yangu. Nataka hii kazi ya Arsenal, ni majukumu makubwa,” alisema Emery.

“Nawaamini wachezaji waliopo hapa...tunaweza kujiongeza na kuwa pamoja kama kikosi. Malengo ni kuwa kitu kimoja na kufanya kazi kwa nguvu zote. Kwa vipaji hivi vilivyopo mahali hapa, tutaweza kushindania mataji. Jambo muhimu zaidi kwenye klabu kwa sasa ni kuirudisha timu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na hilo tunalifanyia kazi. Tunahitaji kuwa sambamba na timu kubwa za England na duniani.”

Kuanza na mastaa watatu

Wakati ripoti zikifichua Emery amepanga kutengeneza timu yake kwa kuwatumia wachezaji; Pierre-Emerick Aubameyang na Aaron Ramsey, kuna mastaa watatu wameripotiwa kuwaniwa kwa haraka na kocha huyo.

Emery amepanga kufanya usajili wa mastaa wa maana na watatu wanaoripotiwa kwamba huenda wakatua Emirates kwa haraka sana ni kipa wa Bayer Leverkusen, Bernd Leno, beki wa Borussia Dortmund, Sokratis Papastathopoulos na kiungo wa Nice, Jean-Michael Seri, ambaye mashabiki wa Arsenal wanamlinganisha na N’Golo Kante wa Chelsea kutokana anavyokaba anapokuwa ndani ya uwanja.

“Nimekutana na Stan na Josh Kroenke na wapo wazi kabisa kwamba wanataka kuleta mafanikio makubwa kwenye timu hii kwa siku za baadaye. Nimefurahi kwa sababu ni kitu ambacho tutakifanya kwa pamoja na kuifanya Arsenal kupendwa na kila mtu,” alisema Emery.

Arsenal imeshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu England iliyomalizika hivi karibuni, ikikusanya alama 37 nyuma ya mabingwa, Manchester City.

Lakini, Emery ameahidi kufanya mambo tofauti kwa usajili wake mpya atakaofanya kwenye kikosi hicho ili kuja kivingine msimu ujao.