Emery aingia Emirates na mikwara mingi

MTU anayeitwa Unai Emery ameingia Arsenal kwa mikwara sana. Sio tu kwa suti maridadi aliyovaa juzi, hapana, ni zaidi ya hivyo unaambiwa.

Ameingia na mikwara kwamba, anataka kuirudisha Arsenal katika nafasi yake inayostahili.

Emery alitambulishwa juzi kuwa kocha mpya wa Arsenal baada ya miaka 22 ya utawala wa Kocha Arsene Wenger klabuni hapo na moja kwa moja amepiga mikwara mingi kwa timu pinzani huku akipania kuirudisha Arsenal katika anga za juu.

Kwanza kabisa, Arsenal ilimaliza nafasi ya sita msimu uliopita huku ikitupwa nje katika nusu fainali ya michuano ya Europa ambayo ingeweza kuwapa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao kama wangechukua. Emery ambaye ni kocha wa KIhispaniola aliyeachana na PSG mwishoni mwa msimu ulioisha amedai atairudisha Arsenal Ligi ya Mabingwa.

“Dhumuni letu kubwa ni kuwa miongoni mwa timu bora Ulaya, kushinda mataji na kuwa timu zinazoogopwa Ulaya. Vile vile nataka mashabiki wajivunie timu yao. Najua tayari wanajivunia lakini nataka wawe zaidi ya hivyo,” alisema Emery.

“Nawaamini wachezaji waliopo. Lengo ni kufanya kazi kwa pamoja. Ni kitu muhimu kwa klabu baada ya kuwa nje ya Ligi ya Mabingwa kwa miaka miwili. Nataka tuwe klabu bora katika Ligi Kuu England, pia duniani.”

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita Arsenal imetwaa mataji matatu tu ya FA na imekuwa nadra sana kwao kuwania ubingwa wa England.

Hata hivyo, Emery alipoulizwa ni namna gani ataifanya Arsenal iwe ya kishindani ndani na nje ya England alionekana kujiamini zaidi.

“Nadhani ni suala la kupambana kuwania ubingwa. Hiki ni kitu ambacho kipo katika historia, pia katika historia yangu. Mataji yote ni muhimu kwetu. Nadhani tunaweza kuwa wagombeaji. Siwezi kuwaahidi leo tutashinda lakini naweza kuwaahidi tutafanya kazi kubwa na tutafanya kwa pamoja. Tutaunganisha hisia zetu na tutapambana kupigania malengo yetu.”

Katika mkutano huo wa kwanza, Emery hakutaka kuzungumzia suala la mipango yake ya uhamisho wa wachezaji katika dirisha hili huku akidai anataka kuzungumza na mchezaji mmoja mmoja kuhusu suala hilo.

“Katika mazungumzo na Ivan Gazidis (bosi mtendaji wa Arsenal) na watu wanaofanya kazi hapa ilikuwa ni muhimu kupata habari za ndani za klabu na kujua ni namna gani tunaweza kuiendeleza hii timu.

“Nawajua wachezaji wote. Nadhani wachezaji wote watakuwa muhimu. Nataka kuongea na wachezaji ana kwa ana,” alisema Emery.

Alipoulizwa kuhusu hatima ya kiungo wa timu hiyo, Jack Wilshere ambaye mkataba wake na Arsenal unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi ujao na atakuwa huru kujiunga na timu nyingine, Emery alihepa swali hilo.

“Sitaki kuongea kuhusu mchezaji mmoja mmoja leo. Hiki kitu ni kikubwa. Huyu ni mchezaji mkubwa,” alikiri Emery ambaye pia aliwahi kuzifundisha Valencia, Sevilla na Spartak Moscow.

Wakati Emery akileta tumaini jipya kwa mashabiki wa Arsenal ambao walichoshwa na utawala wa Arsene Wenger, staa wa zamani wa Arsenal, Martin Keown alidai Emery ana kazi ngumu ya kuirudisha Arsenal katika chati na atalazimika kuwaleta mastaa kama Marco Verrati wa PSG wamsaidie kazi hiyo.

“Kutazamia Emery ataibadilisha timu hiyo kuwa mabingwa ndani ya msimu mmoja, sio kweli. Arsenal imeendeshwa na Wenger kwa miaka 22 na ukiangalia nguvu ya matumizi ya klabu za Manchester upinzani ni mkali,” alisema Keown.

“Kama anaweza kurudisha makali haya basi Arsenal inaweza kupambana kuwania Ligi Kuu England. Mashabiki wanataka kuona timu inapambana, inajituma na iko tayari.

“Emery anahitajika kuchukua wachezaji kama Marco Verratti, ambaye alimfundisha PSG kwa ajili ya kuongeza ubora katika eneo la kiungo,” alisema Keown.