Deal Done Liverpool yaendelea kufungua pochi kikatili

Muktasari:

KUNA kitu Liverpool inakitafuta msimu ujao. Baada ya msimu uliopita kumnasa kiungo, Naby Keita, kutoka RB Leipzig na kumuacha huko huko, kisha msimu huu kumnasa haraka haraka kiungo, Fabinho, kutoka Monaco, sasa ni zamu ya kiungo Nabil Fekir kutoka Lyon.

LIVERPOOL, ENGLAND. KUNA kitu Liverpool inakitafuta msimu ujao. Baada ya msimu uliopita kumnasa kiungo, Naby Keita, kutoka RB Leipzig na kumuacha huko huko, kisha msimu huu kumnasa haraka haraka kiungo, Fabinho, kutoka Monaco, sasa ni zamu ya kiungo Nabil Fekir kutoka Lyon.

Jana Ijumaa mabosi wa Liverpool walikuwa katika hatua za mwishoni za kumnasa kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa dau la Pauni 53 milioni kwa ajili ya kuwa mbadala wa staa wao aliyeondoka kwenda Barcelona Januari mwaka huu, Philippe Coutinho.

Fekir mwenyewe pamoja na kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp na kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, ambaye timu yake inacheza mechi ya kirafiki na Marekani kesho Jumapili, wote wanataka dili hilo likamilike kabla ya kuanza fainali za Kombe la Dunia.

Hadi juzi Alhamisi, Lyon kupitia kwa Rais wake, Jean Michel Aulas, ilikuwa inajaribu kukanusha dili hilo, lakini inaeleweka kwamba staa huyo alikuwa njiani kwenda Anfield na Mkurugenzi wa Liverpool, Michael Edwars alikuwa katika mazungumzo nao kwa ajili ya kukamilisha uhamisho huo.

Kuonyesha kwamba Liverpool imepania kumpata mtu wao, tayari timu ya madaktari wa timu hiyo wanajiandaa kwenda Ufaransa kwa ajili ya kukamilisha vipimo vya afya vya staa huyo katika kambi ya Ufaransa.

Liverpool imeshinda vita ya kumnasa Fekir baada ya Manchester City pia kumtazama staa huyo katika pambano la Europa dhidi ya Everton msimu uliopita, lakini pia aliwahi kuhusishwa kwenda Arsenal katika utawala wa Arsene Wenger.

Endapo Liverpool itakamilisha uhamisho wa staa huyo Mfaransa mwenye asili ya Algeria, basi atakuwa mchezaji wa tatu kwa dau lake kupita Pauni 50 milioni Anfield baada ya dirisha lililopita kumnasa kiungo wa Guinea, Naby keita kwa Pauni 52 milioni kutoka RB Leipzig ingawa walimuacha huko kwa mkopo, lakini pia Januari walimnunua beki, Virgil Van Dijk kwa Pauni 75 milioni kutoka Southampton.

Dau la Fekir pia litaifanya Liverpool kukaribia kufikisha Pauni 100 milioni katika dirisha hili la uhamisho baada ya kumnasa kiungo wa kimataifa wa Brazil, Fabinho kutoka Monaco kwa dau la Pauni 40 milioni.

Baada ya dili la Fekir, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, anatazamiwa kuhamishia nguvu zake kwa kipa wa Roma, Alisson Becker ambaye dau lake linaweza kuvunja rekodi ya uhamisho kwa makipa duniani.

Hata hivyo, italazimika kupambana na Real Madrid ambayo pia inamtaka kipa huyo anayetazamia kukaa katika lango la Brazil katika Kombe la Dunia nchini Russia.

Klopp hana imani na makipa wawili wa Liverpool, Simon Mignolet na Hugo Loris, ambaye alifanya makosa makubwa katika pambano la fainali za Ulaya dhidi ya Real Madrid nchini Ukraine na Klopp amedhamiria kupata kipa wa kiwango cha juu katika dirisha hili.

Klopp pia ameanza kuhusishwa kumnasa kiungo wa Stoke City, Xherdan Shaqiri, ambaye anaruhusiwa kuondoka klabuni hapo kwa dau la Pauni 12 milioni tu baada ya timu hiyo kushuka daraja.

Liverpool inatazamiwa kuanza mazoezi ya msimu mpya Julai 12 na mechi yao ya kwanza ya maandalizi ya msimu mpya inatazamiwa kuwa dhidi ya Chester Jumamosi inayofuata huku wachezaji watakaokuwa wametokea Kombe la Dunia wakitazamiwa kuongezewa muda zaidi wa likizo.