Liverpool yaipunguza kasi Man United

Muktasari:

Vijana wa Jurgen Klopp walikuwa katika kiwango cha juu katika muda wote wa mchezo huo na kulishambulia lango la Man United na mashuti yao 19 yakiishia mikononi mwa kipa David de Gea aliyekuwa katika kiwango bora.

Liverpool, England. Liverpool itajilaumu wenyewe kwa kukubali kulazimishwa suluhu na Manchester United pamoja na kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield.

Vijana wa Jurgen Klopp walikuwa katika kiwango cha juu katika muda wote wa mchezo huo na kulishambulia lango la Man United na mashuti yao 19 yakiishia mikononi mwa kipa David de Gea aliyekuwa katika kiwango bora.

Moja ya nafasi za wazi walizokosa ni ile ya kipindi cha kwanza wakati kipa De Gea alipopangua shuti akiwa yeye na Joel Matip kabla ya Mohamed Salah kupoteza nafasi hiyo kwa kupiga shuti nje.

Man United ilijibu mapugo kwa shambulio la kushtukiza kupitia mshambuliaji wake Romelu Lukaku aliyepiga shuti kali akiwa yeye na kipa Simon Mignolet wa Liverpool akapangua mpira.

Matokeo hayo yanaendeleza rekodi mbaya ya Jose Mourinho akiwa ameshinda mechi moja kati ya nane alizocheza dhidi ya Mjerumani Jurgen Klopp katika mashindano yote.