Conte kapiga mkwara

Muktasari:

Mtaliano huyo amesema Chelsea itakuwa imepoteza mshindi wa kweli kama wataamua kumfukuza kazi. Chelsea ilibeba ubingwa wa Kombe la FA juzi Jumamosi, ikiwa miezi 12 imepita tangu ilipobeba ubingwa wa Ligi Kuu England.

UKISHINDA unakuwa na raha sana. Ndivyo ilivyo kwa Atonio Conte amewachimba mkwara Chelsea baada ya kuwaambia watafanya makosa makubwa kama wataamua kumfuta kazi.

Mtaliano huyo amesema Chelsea itakuwa imepoteza mshindi wa kweli kama wataamua kumfukuza kazi. Chelsea ilibeba ubingwa wa Kombe la FA juzi Jumamosi, ikiwa miezi 12 imepita tangu ilipobeba ubingwa wa Ligi Kuu England.

Kwa miezi kadhaa sasa, Conte amekuwa akitajwa huenda akafunguliwa mlango wa kutoka huko Stamford Bridge hasa baada ya msimu huu kumalizika na Chelsea kumaliza ligi nafasi ya tano na kukosa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

“Msimu mgumu kama huu, bado nimeonyesha mimi ni mshindi wa kweli.

Huo ndio ukweli, msimu huu umenipa maana kubwa kuliko ushindi wangu wote niliowahi kupata huko nyuma.”

Conte, ambaye analipwa mshahara wa Pauni 9 milioni kwa mwaka, anampa mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich changamoto kuhusu kumfuta kazi baada ya kuiongoza timu hiyo kwa misimu miwili na yote amefanikiwa kubeba mataji. “Nina mkataba na nitaendelea kujitolea kwenye timu hii. Achana na ule uvumi ulioanza kuzagaa tu baada ya kufungwa mechi ya kwanza tu dhidi ya Burnley. Baada ya miaka hii miwili, nadhani klabu itakuwa inanifahamu vizuri. Mimi ni mshindi wa kweli.”