Conte awataka mabosi Chelsea kumfukuza kazi

Muktasari:

Conte ametoa kauli hiyo baada ya Chelsea kuogelea mvua ya mabao 4-1, dhidi ya Watford katika mchezo wa Ligi Kuu England.

London, England. Kocha wa timu ya Chelsea Antonio Conte, amesema yuko tayari kufukuzwa kazi.

Conte ametoa kauli hiyo baada ya Chelsea kuogelea mvua ya mabao 4-1, dhidi ya Watford katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Kocha huyo ameitaka bodi ya klabu hiyo kumfukuza kutokana na matokeo ya juzi usiku ikiwa ugenini.

Pia kocha huyo wa zamani wa ‘Kibibi Kizee’ cha Turin Juventus, amehoji ubora wa wachezaji wake kama wana sifa za kucheza Chelsea.

Mtaliano huyo amekuwa na mzozo usiokwisha na mabosi wa Chelsea kutokana na misimamo yake ndani ya klabu hiyo.

Matokeo hayo ni mabaya zaidi kwa timu hiyo ndani ya wiki moja na huenda mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich ambaye amekuwa kimya muda mrefu akatoa tamko.

Kocha huyo alisema hana hofu kama atafukuzwa Chelsea kama bodi itamuona ni tatizo.

Hii si mara ya kwanza kocha huyo kutoa kauli za kutatanisha kuhusu hisia zake kwa mabosi wake tangu alipoibua mzozo na Diego Costa.

Bodi ya Chelsea inamuona Conte ni kocha mwenye msimamo na asiyetaka ushauri katika masuala ya kiufundi.

Mbali na vigogo hao, kocha huyo anadaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya wachezaji waandamizi wa kikosi hicho.

“Sina hofu, sina hofu na kibarua changu. Ninafanya kazi kila siku tena kwa asilimia 120. Sawa? Inatosha, sawa kama vipi klabu inaweza kuchukua uamuzi tofauti, lakini siogopi,” alisema Conte.

Kocha huyo alidokeza anapata usingizi bila presha kwa kuwa amejitahidi kufanya kazi vyema kama Chelsea itaamua kumfukuza hakuna tatizo maisha yataendelea.